Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wakandarasi Watakiwa Kukamilisha Miradi Kwa Wakati Katika Mji Wa Serikali, Mtumba


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya Mji wa Serikali, Mtumba, ili kuimarisha utoaji wa huduma za Serikali na kuongeza ufanisi wa utendaji wa taasisi za umma. Amesisitiza kuwa utekelezaji wa azma hiyo unategemea pia wakandarasi kukamilisha miradi wanayopewa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa.

Prof. Kabudi amesema hayo leo, tarehe 19 Juni, 2026, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma. Alieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika ujenzi wa majengo ya Wizara, taasisi na miundombinu muhimu.

Amesema uwekezaji mkubwa uliofanyika jijini Dodoma, hususan katika Mji wa Serikali, unaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha makao makuu ya nchi kwa viwango vya kimataifa. Kutokana na mafanikio hayo, Prof. Kabudi amesema kuna kila sababu ya kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na uamuzi wa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya Mji wa Serikali.

Katika ziara hiyo, Waziri Kabudi alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), ambapo aliwataka wakandarasi wa Suma JKT kwa kushirikiana na vikosi vyote vya ujenzi kuongeza kasi, ubora na ufanisi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Aidha, alikagua mradi wa majisafi na mfumo wa ukusanyaji na uondoshaji wa majitaka katika Mji wa Serikali unaotekelezwa na Kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited (CHEC) chini ya usimamizi wa NORPLAN. Akiwa katika eneo la mradi, alimtaka mkandarasi kuzingatia viwango vya ubora na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili kuwezesha majengo ya Serikali kutoa huduma kwa ufanisi.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi, akiwa ameambatana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba, pamoja na wajumbe wa Bodi ya Benki hiyo, walikagua kiwanja cha Benki Kuu ya Tanzania kilichopo katika Mji wa Serikali. Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Ofisi za Benki Kuu katika eneo hilo.

Ziara ya Prof. Kabudi ni sehemu ya utaratibu wa Serikali, chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu,  kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa ubora unaokusudiwa na kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wananchi.