Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tanzania yaahidi kuendeleza ushiriano na Burundi sekta ya nishati


Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na nchi ya Burundi katika nyanja mbalimbali za maendeleo zikiwemo za kijamii na kiuchumi kupitia mipango thabiti ya usambazaji wa nishati ya miongoni mwa nchi hizo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika mazungumzo yake na Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Mhe Ibrahim Uwizeye aliyemtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

"Rais Samia ni kinara katika kujenga mahusiano na ndani ya nchi na kimataifa, kama ilivyo kwa uhusiano kati yetu na Burundi ambayo  imewezesha kutekeleza miradi kadhaa ukiwemo mradi wa umeme wa RUSUMO unaoendeshwa kwa ubia wa nchi Tatu za Rwanda, Burundi na Tanzania" Amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na nchi hiyo na kuwataka kuimarisha mahusiano kwa wafanyabiashara ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza kwa wananchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini wa Burundi, Mhe. Uwizeye amemshukuru Rais Samia kwa utayari wa kuisaidia nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo nishati.

Dkt. Biteko amekutana na Waziri wa Nishati wa Malawi na ujumbe wake, Waziri wa Nishati wa Tunisia, Waziri wa Nishati wa Rwanda, Waziri wa Nishati wa Comoro na Rais wa kampuni ya GE VERNIVA ambao kwa nyakati tofauti wamezungumzia maaendeleo na ushirikiano katika sekta ya nishati.

Mazungumzo haya yamekuja ikiwa ni siku moja baada ya Mkutano wa Nishati Barani Afrika unaojulikana kama misheni 300 unaolenga kuwawezesha waafrika milioni 300 barani Afrika kunufaika na nishati ya umeme ifikapo mwaka 2030.

MWISHO=