Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali ya Zambia Yapata mafunzo Kutoka Tanzania: Yapongeza Ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma


Maofisa waandamizi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Zambia wametembelea Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza namna Tanzania ilivyofanikiwa kutekeleza mradi mkubwa wa kitaifa wa kuhamishia shughuli za serikali katika mji huo.

Wakiwa katika ziara hiyo, maofisa hao walipokelewa na Mratibu wa Ujenzi wa Mji wa Serikali, Bw. Noel Mlindwa, ambaye alieleza kuwa Tanzania imeweka historia kwa kuanzisha na kutekeleza kwa mafanikio makubwa ujenzi wa mji wa serikali, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Bw. Mlindwa alifafanua kuwa mji huo umejengwa kwa kuzingatia mipango bora ya kisasa, usimamizi makini wa rasilimali na matumizi ya teknolojia, hali iliyowavutia wageni hao kutoka Zambia.

Kwa upande wao, maofisa wa Zambia waliipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua kubwa ilizopiga na walisisitiza kuwa Mji wa Serikali Dodoma si tu ni kielelezo cha maendeleo, bali pia ni kivutio cha kiutalii na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine barani Afrika.