Habari
Mitambo nane katika Mradi wa JNHPP imeshakabidhiwa kwa Serikali - Dkt. Biteko
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mitambo nane kati ya tisa ya kuzalisha umeme katika Mradi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) tayari imekabidhiwa kwa Serikali baada ya kuwashwa na hivyo imebakia mashine moja tu ambayo itakuwa tayari mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2025.
Aidha, Dkt. Biteko ametaja ongezeko la wadau ambao wako tayari kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa umeme Afrika.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Januari 31, 2025 wakati akichagia Azimio la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Nishati Afrika (Mission 300) uliyofanyika Januari 27 na 28, 2025 jijini Dar es Salaam.
“Benki ya Dunia imetoa ahadi ya dola za kimarekani bilioni 22, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) dola bilioni 18.2, Benki ya Maendeleo ya Kiislamu dola bilioni 2.7, Benki ya Maendeleo ya Asia dola bilioni 1.5, Benki ya Maendeleo ya Ufaransa dola bilioni 1 na wafadhili wengine lukuki.” Amesema Dkt. Biteko.