Habari
Miradi iendane na thamani ya fedha inayotumika-Majaliwa
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wahandisi wazawa kuhakikisha miradi wanayoisimamia inakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na iendane na thamani ya fedha inayotumika.
Amesema ni wajibu wa Wahandisi kuisaidia Serikali kuokoa fedha kwa kukadiria fedha inayohitajika kulingana na thamani ya mradi husika.
"Nitumie fursa hii kuwasihi wahandisi muendelee kufuata miiko na maadili ya taaluma hii ili kulinda heshima ya taaluma hii lakini pia kulinda pato la nchi ambalo linatengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi."
Ameyasema hayo leo Jumanne 27, Agosti 2024 alipomuwakilisha Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sherehe za Kuadhimisha Miaka 50 ya Idara ya Ujenzi ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST).
"Uhandisi ni taaluma yenye miiko na inayopaswa kuzingatia maadili. Miongoni mwa miiko na maadili hayo ni kuhakikisha kuwa miradi mnayoisimamia inakidhi viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa na inaendana na thamani ya fedha inayotumika."
Aidha, amewataka waajiri wote nchini kuweka utaratibu wa kuajiri wahandisi wahitimu wa ndani na kuwajengea uwezo wakati wakiwa kazini pamoja na kushirikiana na taasisi za mafunzo kutenga nafasi na kuwapokea vijana waliopo mafunzoni ili kuwapatia uzoefu wa kazi.
"Utaratibu huu ni kwa manufaa ya Taifa na kwa waajiri pia kwa kuwa vijana watahitimu wakiwa wameiva kitaaluma na kiutendaji."
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Taasisi ya Sayansi ya Teknolojia ya Karume na taasisi nyingine za mafunzo nchini zihakikishe zinazalisha wahitimu wengi wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
"Kwa kufanya hivi ,tutaongeza kiwango cha kazi za kibobezi zinazofanywa na wazawa hivyo kupunguza matumizi ya wataalamu wa kigeni na ikibidi wageni watumike zaidi katika kujenga uzoefu na kuimarisha uwezo wa Watanzania."
Kwa Upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Lela Mohamed Mussa (MB), amesema Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Hussein Mwinyi ameanzisha programu ya kutoa fedha kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa fani za Uhandisi na kutoa ufadhili na mafunzo ya amali pamoja na kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa fani hiyo.
"Kwa kuzingatia umuhimu wa fani ya uhandisi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia mpango wake wa Mageuzi ya Elimu imeanza kusomesha masomo ya Mafunzo ya Amali kuanzia ngazi ya Sekondari ambayo yatashajihisha na kutoa muelekeo wa kitaaluma (carrier path) kwa wahitimu kujiunga na Vyuo vya Ufundi vya Elimu ya Kati ikiwemo KIST. Hili litatoa fursa zaidi kwa vijana wengi kujiunga katika fani za uhandisi."
Naye, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda amesema Wizara zote zimekuwa na Ushirikiano wa kuwezesha wanafunzi wa fani za Uhandisi ili kuongeza tija katika mafunzo wanayopata.
Awali, Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Karume(KIST) Dkt. Mahmoud Abulwahab Alawi,amesema chuo hicho kimeanzisha fani mbalimbali zinazoendana na Sera za Serikali ikiwemo Sera ya Uchumi wa buluu na maboresho ya sekta ya afya.
"Serikali zetu zote mbili zimekuwa zikiimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kufanya matengenezo hospitali na vituo vya afya katika mikoa na wilaya mbali mbali nchini pamoja na kuvipatia vifaa tiba vya kisasa."
Amesema Katika kuunga mkono jitihada hizo, Taasisi imeanzisha fani ya Uhandisi Umeme na Vifaa Tiba (Electrical and Biomedical Engineering) kwa ngazi ya Stashahada kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Jambo ambalo litasaidia kupata wataalamu wabobezi wa kuvifanyia matengenezo vifaa hivyo pale inapohitajika.
Aliongeza kuwa katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Buluu, Taasisi imeanzisha fani ya Usindikaji wa Mazao ya Baharini (Aquatic Product Processing Technology) kwa kiwango cha Stashahada, ambapo mkupuo wa kwanza unatarajiwa kuhitimu mafunzo yao Novemba 2025 na wahitimu kuweza kupata fursa za kujiajiri na kuajiriwa.