Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Makatibu Wakuu Wateta Mikakati ya Kuendeleza Safari Channel ya TBC


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. James Kilabuko, ameongoza kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali kilichofanyika leo jijini Dodoma kwa lengo la kujadili namna bora ya kuimarisha uendeshaji wa Tanzania Safari Channel chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Kilabuko amesema chaneli hiyo imekuwa nyenzo muhimu ya kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia vivutio vya utalii vilivyopo nchini, hivyo ni muhimu kwa taasisi zote za serikali kushirikiana katika kuiendeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba Chacha, akiwasilisha taarifa kuhusu chaneli hiyo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusaini sheria mpya ya TBC, ambayo imefungua milango ya maboresho ya kiutendaji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa umma.

Chaneli ya Tanzania Safari Channel imekuwa chombo mahsusi cha kuitangaza Tanzania kama nchi yenye vivutio vya kipekee duniani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimkakati kukuza sekta ya utalii.