Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 556 hadi 104


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2020 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 Februari, 2025.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano navyo vimepungua kutoka 67 mwaka 2020 hadi 43 Februari, 2025.

Amesema hali hiyo imetokana na jitihada za kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini, unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi. “Jitihada  hizo zimewezesha kuongezeka kwa  vituo vya kutolea huduma za afya kutoka vituo 8,458 mwaka 2020 hadi vituo 9,826 Februari, 2025.”

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Aprili 9, 2025) alipowasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Mtumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2025/2026 Bungeni jijini Dodoma.

Vilevile, Waziri Mkuu amesema idadi ya hospitali zinazotoa huduma ya magonjwa ya dharura zimeongezeka kutoka saba mwaka 2020 hadi 116 mwaka 2025. “Pia, vituo vya kutolea huduma za afya vyenye majengo ya mama na mtoto vimeongezeka kutoka 6,081 mwaka 2020 hadi 7,397 Februari, 2025.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema, Serikali imeendelea kutekeleza mipango na mikakati mahsusi ya kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini.

Amesema mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga; huduma za afya ya uzazi na mtoto; kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya; pamoja na kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya; Mifumo ya TEHAMA inayowezesha utoaji wa huduma za afya, matumizi ya takwimu, utawala bora na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya katika ngazi zote.

Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali katika mwaka 2025/2026, itaendelea kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa; kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema huduma nyingine zitakazoendelea kuimarishwa kuwa ni pamoja mifumo ya ugharimiaji wa huduma za afya nchini; huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto; huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini; na kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa UKIMWI bado ni tishio, takwimu zinavyoonesha kuwa kiwango cha maambukizi mapya ni watu 60,000 kila mwaka na takribani asilimia 34.3 ya  wanaopata maambukizi mapya ni vijana.

Amesema katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kuratibu shughuli za UKIMWI kwa kutoa huduma endelevu na stahimilivu kwa WAVIU; kuimarisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI ili uweze kufanikisha malengo ya nchi katika kutokomeza UKIMWI ifikapo 2030.

Amesema msukumo mkubwa utawekwa katika kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto; kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

“Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, watu 1,536,842 kati ya watu 1,690,948 wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) walikuwa wanatambua hali zao za maambukizi.

Kadhalika, WAVIU 1,545,880 wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU ambapo watu wazima wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni asilimia 96.4.”

Sambamba na hayo, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua mabadiliko ya sera za misaada kutoka kwa baadhi ya wafadhili wa masuala ya UKIMWI na inachukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha uwekezaji kwenye eneo la utaoji huduma kwa WAVIU.

Amesema hatua hizo zina lengo la kuwezesha Taifa kujitegemea na zitaendelea kuchukuliwa katika maeneo mengine. “Niwahakikishie Watanzania wote, kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha huduma zinazohusiana na masuala ya UKIMWI zinaendelea kupatikana na hakuna Mtanzania hata mmoja atakayekosa huduma hizo.”