Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Maambukizi Mapya VVU Yaendelea Kushuka


Imeelezwa kwamba takwimu za maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI katika kipindi cha miaka mitano imeendelea kushuka kulingana na matokeo ya utafiti yaliyofanywa hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dkt. Catherine Joachim leo Jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka katika Wizara za Kisekta na Taasisi ili kuangalia mpango  uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI.

Dkt. Catherine amebainisha kuwa, nchi imefanya vizuri kwa takwimu za maambukizi mapya zilizotoka mwaka (2023-2024) ambapo maambukizi mapya yalikuwa watu 60000 kwa mwaka ukilinganisha na kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo maambukizi haya yalikuwa watu 72000 kwa mwaka.

“Halikadhalika ukiangalia vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa Matokeo ya Utafiti ya Mwaka (2023-2024) watu 24000 walifariki kulinganisha na watu 28000 waliokuwa wamefariki mwaka (2016-2017),” aliongeza Dkt. Catherine.

Ameongeza kusema, ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU umepungua kutoka 14% hadi kufikia 5%, hatua ambayo ni muhimu kwa sababu inaongeza muitikio wa watu kupima na kujua afya zao.

Aidha, ilikuendelea kuimarisha mapambano, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania imekutana na Wakurugenzi wa Sera na Mipango kutoka katika Wizara za kisekta na Taasisi ili kuangalia mkakati wa  usimamizi na utawala kutoka ngazi ya msingi mpaka ngazi ya Taifa kwa kuangali gharama ya fedha za UKIMWI kulingana na mikakati ya Serikali katika kuongeza fedha za ndani ya Nchi na kutoka kwenye Sekta Binafsi.

Vilevile, Dkt. Catherine alisema “tutaangalia namna ya kuimarisha utoaji wa huduma na mifumo ya afya na kuongeza uwajibikaji wa wananchi wenyewe katika muitikio”.