Habari
Jumuiya ya umoja wa Ulaya yashirikiana (eu) na Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Kigoma.
Ofisi ya Waziri Mkuu-Sera, Bunge na Uratibu na wenye Ulemavu kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imeanza utekelezaji wa mradi wa Mwitikio wa Kikanda dhidi ya Uhamaji Unaotokana na Mabadiliko ya Tabia nchi (Regional Responses to Climate Displacement in Subsaharan Africa- RE2CLID) unaolenga kujenga uhimilivu wa jamii zinazoishi maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mradi huo unafadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya(EU) Unatekelezwa na mashirika ya IOM UN migration, Enabel na kusimamiwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara za kisekta pamoja na Mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile RedCross umezinduliwa rasmi na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Bw. Vonyvako Luvanda kwaniaba ya Naibu Katibu Mkuu Dkt.James Kilabuko, katika Hoteli ya Morena, Jijini Dodoma.
Akizungumza katika uzinduzi huo Bw. Luvanda amesema, mradi huo unalenga kusaidia jamii zilizoathirika na kuhamishwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika pamoja na kuimarisha mifumo ya uratibu wa maafa na usimamizi wa rasilimali za asili.
Pia, ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2025 hadi Septemba 2029 utaongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi huku ukipewa kipaumbele na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania Bw. Marc Stalmans amesema EU imefadhili mradi huo wenye thamani ya Euro milioni 13 kwa lengo la kusaidia jamii zilizoathirika zaidi na mabadiliko ya tabia nchi, hususan wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika.
Ameongeza kuwa, ongezeko la kina cha maji limeharibu makazi, mashamba, barabara pamoja na huduma muhimu kama maji safi na umeme, hali inayosababisha wananchi wengi kupoteza maeneo yao ya kuishi.




