Habari
Dkt. Yonazi Ashukuru michango inayoendelea kutolewa, afafanua namba sahihi ya kutuma michango Maafa Kariakoo
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera,Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea kujitolea na kutoa michango kwa ajili ya maafa ya Kuporomoka kwa ghorofa eneo la Kariakoo kusema ni moyo wa upendo unaoneshwa kwa matendo mbalimbali walioguswa na maafa hayo.
Ametoa shukrani hizo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hatua zinavyoendelea katika eneo lililopatwa na ajali ya kuporomoko kwa jengo la ghorofa mtaa wa Agrey Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Dkt. Yonazi ametumia nafasi hiyo kutangaza “Control Number” kwa ajili ya kuwawezesha wananchi ambao wataguswa na maafa hayo kwa kutuma michango yao kwa ajili ya kuendelea kusaidia katika hatua baada ya kutokea maafa hayo.
" Control number ni 987320001709 ambapo namba hii inatumika kwa mitandao yote ,mwananchi anaweza kuchangia kuanzia 1000 na kuendelea na fedha hizi zinaingia moja kwa moja kwenye akaunti ya Maafa au kuchangia kupitia akaunti ya National Relief Fund yenye namba 9921159801 ambayo ipo Benki Kuu ya Tanzania,” amesema Dkt.Yonazi.
Kwa hatua nyingine Dkt. Yonazi amepokea msaada kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lililokabidhi kiasi cha shilingi za Kitanzania Milioni Ishirini kwa lengo la kusaidia kufuatia maafa hayo.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya TANAPA, Jenerali mstaafu George Waitara amesema kuwa tukio hilo limesababisha maafa makubwa ikiwemo vifo,uharibifu wa mali pamoja na matatizo ya kisaikolojia kwa waathirika wa tukio hilo.
"TANAPA ni sehemu ya wananchi wa Tanzania,hivyo janga hili tumetugusa tukaona tutoe chochote kusaidia uokoaji wa maafa haya na Watanzania wasiwe na taharuki kwani tumeona shughuli za uokoaji zinakwenda vizuri, kikubwa wawe wanafuatilia taarifa kupitia mamlaka husika na si vyanzo vingine " amesema Jenerali Mstaafu Waitara.