Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu: Viongozi chepeni kazi, msisubiri teuzi


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi na watendaji nchini wachape kazi na waendelee kutekeleza majukumu yao badala kusubiri teuzi (maarufu kama pdf ama mkeka).

Amesema zipo taarifa zinazoonesha kuwa baadhi ya viongozi wamepunguza kasi ya utendaji wakisubiri kile kinachoitwa “mkeka”, “PDF” hali inayosababisha huduma za umma kudorora. “Wabainishwe wanaosubiri mkeka na wale wanaosubiri PDF, tuwatoe ili tuwaweke watu wanaotaka kufanya kazi. Hatutaki shughuli za ofisi za umma zisimame kwa sababu kuna watu wanasubiri mkeka,” amesema.

Ametoa wito huo bungeni jijini Dodoma leo (Ijumaa, Juni 26, 2026) wakati akihitimisha mkutano wa tatu wa Bunge ambalo limeahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu.

Amesisitiza kuwa viongozi wote wanapaswa kuendelea kutekeleza majukumu yao ipasavyo, huku akionya kwamba wale watakaobainika kusubiri teuzi badala ya kuwahudumia wananchi wataondolewa na nafasi zao kuchukuliwa na watu wenye utayari wa kufanya kazi.

“Zipo tetesi katika baadhi ya maeneo kwamba viongozi wapo kama wamepigwa ganzi. Wanasubiri nini? Eti PDF. Mkeka. Teuzi. Haya ni mambo ya ajabu. Kuwa ofisini na kusubiri teuzi ni mambo ya ajabu,” amesema.

Akifafanua suala la utatuzi wa kero za wananchi badala ya kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa, Waziri Mkuu amesema ziara hizo katika maeneo mbalimbali nchini ni sehemu ya majukumu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa shughuli za serikali ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi. “Katika ziara hizo wananchi wengi wamekuwa wanajitokeza kuwasilisha kero mbalimbali lakini baadhi ya kero hizo, zilitarajiwa ziwe zimetatuliwa na viongozi waliopo kwenye mamlaka za serikali za mitaa,” amesema.

“Ninawakumbusha viongozi na watumishi wote wa umma kwamba utatuzi wa kero za wananchi ni sehemu ya majukumu yao ya kila siku. Aidha, ziara za viongozi wa Kitaifa ikiwemo ziara ya Waziri Mkuu siyo mbadala wa kutoa huduma hizo kwa wananchi.”  

Waziri Mkuu amezielekeza Wizara, Idara, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe Mifumo iliyopo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya mtaa na kijiji inatoa huduma kwa wananchi ipasavyo.

Vilevile, amewataka viongozi na watendaji katika kila ngazi wasimamie na kutekeleza kwa ukamilifu maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa kitaifa kwenye ziara ikiwemo kutatua na kusikiliza kero za wananchi. “Taasisi zote zitenge muda wa kusikiliza changamoto za utoaji huduma katika maeneo yao. Ufuatiliaji unaendelea kufanyika na viongozi  watapimwa kwa namna wanavyotekeleza maagizo hayo,” amesema.

Akielezea migongano kwenye usimamizi wa shughuli katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu amesema kila mwaka Serikali inaingia gharama za uchaguzi ambapo viongozi na watendaji wanakuwa katika mchakato wa uchaguzi. Amesema mazingira hayo yanazorotesha utendaji, yanachochea migongano na kuondoa utulivu kwenye mamlaka za serikali za mitaa na hivyo yatafanyika mabadiliko ya kuondoa chaguzi hizo.

“Katika mkutano ujao, Serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria kuhusu nafasi za Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri. Tutaondoa uchaguzi kufanyika kila mwaka. Lengo ni kubadilisha mfumo wa sasa na kuwa na Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti kuwa kiongozi kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza la Madiwani. Marekebisho hayo yanatarajia kuleta utulivu, ili viongozi wajikite katika kufanya kazi na kujiekeleza kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezielekeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii wahakikishe wanawarejeshea  wafugaji mifugo yao walioshinda kesi mahakamani.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa baadhi ya wafugaji katika maeneo mbalimbali walitaifishiwa mifugo yao baada ya kukamatwa katika maeneo yaliyohifadhiwa. “Tekelezeni maamuzi yaliyotolewa na mahakama kwa kuwarejeshea mifugo yao wafugaji walioshinda kesi mahakamani. Na kama mifugo hiyo ilikufa au ilipotea, basi wawarejeshee fidia ya mifugo yao,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema kuwa mashauri hayo yalikwishahitimishwa katika vyombo vya kisheria, ambapo wafugaji walipata ushindi na kuamriwa kurejeshewa mifugo yao. “Mpaka sasa taasisi husika hazijatekeleza maamuzi hayo ya mahakama. Badala yake wameishia kuwaambia wafugaji kuwa mifugo yao ilikufa, ilipotea, au kutoa sababu nyingine. Vitendo hivyo vinadhoofisha sekta ya mifugo na kuwaacha wananchi hawa katika ufukara.”

Amesema ili kuimarisha misingi ya utawala wa kisheria na utoaji haki kwa wananchi, kupitia mkutano ujao wa Bunge, Serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria zinazosimamia utaifishaji mifugo na mali kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na itaenda kufutwa.