Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Biteko asema Tanzania ina usalama wa chakula, awapongeza wakulima


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wakulima nchini kwa jitihada zao za kuzalisha mazao kwa wingi na hivyo  kusaidia nchi kuwa na usalama wa chakula  ikiwa ni pamoja na kuwezesha sekta ya kilimo kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo leo Julai 5, 2025 jijini Dodoma wakati akifunga Kongamano la Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani.

“Leo sekta ya kilimo ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu, tunazungumza mchango wa GDP wa asilimia 26, tunazungumza mazao ambayo yanatupa  usalama wa chakula katika nchi yetu, nchi zingine zinahangaika kupata chakula sisi watu wetu wana uhakikia wa kupata chakula mitaani kwa sababu wakulima wamewezeshwa kufanya biashara ya kilimo, ” amesema Dkt. Biteko

Amebainisha kuwa takwimu zinaonesha  utendaji wa vyama vya ushirika  umeendelea kuimarika kila wakati mauzo ya nje   yameongezeka. Ambapo kwa mwaka 2024/2025 jumla ya vyama vya ushirika 1,084 viliuza kahawa na tumbaku moja kwa moja nje ya nchi kiasi cha Dola za Marekani 344,800,000 ikilinganishwa na Dola za Marekani 325,500,000 kwa mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la Dola za Marekani 19,300,000.

Dkt. Biteko amefafanua kuwa Vyama vilivyopata Hati safi ya Ukaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi la Vyama vya Ushirika (COASCO) vimeongezeka kutoka vyama 339 mwaka 2021/2022 hadi kufikia vyama 631 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la vyama 292 ambayo ni asilimia 86.13

Aidha, Vyama vilivyopata Hati isiyoridhisha vimepungua kutoka Vyama 1,198 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Vyama 263 mwaka 2023/2024 sawa na upungufu wa vyama 935 ambayo ni asilimia 78.

Ametoa rai kwa Vyama kuwawezesha wanawake kwa kuweka mikakati mbalimbali ili idadi ya Vyama vya Ushirika vya Wanawake iongezeke kutoka Vyama 50 vilivyopo sasa.

Licha ya mafanikio hayo katika sekta ya kilimo, Dkt. Biteko ameziagiza Wizara za Fedha na Kilimo kupatia ufumbuzi masuala ya bei ya mazao ya wakulima, pembejeo na mahitaji ya msingi ya wakulima ili kuendelea kufanya kilimo chenye tija.

 “Serikali ya awamu ya Sita inatambua kwamba Ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika kuunganisha nguvu zao na kujiendeleza kiuchumi. Hivyo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi na jitihada zote zenye lengo la kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinasonga mbele kiuchumi na kijamii, ” amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Vyama vya Ushirika vimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi ndio sababu Rais  Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipa msukumo mkubwa sekta ya kilimo. Pia amempongeza Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe kwa kuhakikisha sekta hiyo inatimiza maoni ya Rais Samia ya kuwainua wakulima kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi.

Vilevile, amempongeza Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege kwa kuwasema wakulima nchini na hivyo kuboresha  utendaji kazi wa Vyama vya Ushirika huku akivitaka Vyama hivyo kuwa na viwanda vya uchakataji wa mazao  ili kuongeza thamani ya bidhaa na kuongeza wigo wa masoko.

Naye, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada mbalimbali za  kuboresha sekta ya kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo, kutoa zuruku za  mazao na kuanzisha kwa Taasisi mbalimbali ikiwemo COPRA zinazolenga kutetea maslahi ya wakulima nchini.

Aidha, Mhe. Bashe amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo ya vijijini kama vile uwepo wa umeme katika vijiji vyote nchini na barabara unachochea maendeleo vijijii na hivyo hutoa fursa kwa wakulima kuanzisha mashine za uchakataji mafuta mfano ya alizeti na kusafirisha mazao yao.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa huo sasa una Vyama vya Ushirika 244 na kwa sasa wananchi wamejua umuhimu wa vyama hivyo  hususan  lengo namba saba la kuvitaka kushirikiana na jamii.

Akitoa taarifa ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25 ya hali ya Vyama vya Ushirika nchini, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege ametaja mafanikio kadhaa yaliyopatika ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Ushirika katika mikoa minne nchini

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Bw. Tito Haule amesema kuwa Maadhimisho hayo kwa mwaka 2025 wanaushirika nchini wanaungana na wadau wengine duniani hivyo kufanya kuwa Maadhimisho ya 102 tangu kuanzishwa.

Bw. Haule ametaja baadhi ya malengo ya mwaka wa Ushirika 2025 kuwa ni pamoja na kutoa fursa kwa Vyama Vya Ushirika kuonesha bidhaa zao kwa jamii na kuhabarisha umma juu ya mchango wa Vyama hivyo na kuhimiza uwepo wa sera na desturi

Aidha, amesema baadhi ya mafanikio ya Vyama Vya Ushirika nchini ni ongezeko la idadi ya  wanachama  kutoka milioni 6.9 mwaka 2021/22 hadi kufikia milioni 10, kuongeza ajira za kudumu na mikataba kwa vijana na kuchangia pato la kodi kwa Serikali hadi shilingi bilioni  9.5 mwaka 2020/22 na shilingi bilioni 12.5 mwaka 2023.

Pia, ameishukuru Serikali kwa kuongeza mtaji wa shilingi bilioni 5 katika Benki ya Ushirika na kuimarisha Vyama Vya Ushirika kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA.

Mwisho.