Habari
WFP kuendelea kushirikiana na Idara ya Menejimenti ya Maafa nchini
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula la Duniani (World food Programme -WFP) limesema litaendeleza mashirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha masuala ya menejimenti ya maafa yanaendelea kutekelezwa kwa tija na malengo yaliyokusudiwa kwa kuimarisha uwezo wa kitaalamu na Kiteknolojia kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Hayo yameelezwa na Naibu Mkurugenzi wa shirika hilo Bw. Brian John Bogart alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ofisi kwake jijini Dodoma.
Amesema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano hususani katika kuwajengea uwezo juu ya matumizi vifaa vya kiteknolojia ya kisasa ya kuchukua matukio na tarifa mbalimbali kwa kutumia vifaa aina ya Ndege Nyuki (drones) pamoja na kufadhili vifaa hivyo.
Aidha wataendelea kutoa mafunzo kuhusu masuala ya uchambuzi wa taarifa (Data Analysis) ili kuwa na utaalamu wa kutosha katika kuchambua taarifa zinazokusanywa kupitia vifaa hivyo (drones) kwa ajili ya kuboresha na kuwa na ufanisi zaidi kwa kutumia teknolojia hiyo ya kisasa.
"Tumeendelea kutoa elimu na tutafanya mafunzo kwa wataalam wetu ili kuwa na ujuzi katika kuchambua taarifa pamoja na matumizi ya drone na kuzitafsiri taarifa kama inavyotakiwa," alielezaNaye Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dkt. Jim Yonazi aliwashukuru WFP huku akisema Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano hasa katika kipindi hiki cha mvua nyingi zenye kuleta maafa nchini kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa na matukio hayo.
"WFP mmeendelea kuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali hususani katika masuala ya Menejimenti ya Maafa, niendelee kutoa wito kwa wadau wengine pia kuunga mkono jitihada za Serikali katika masula mbalimbali nchini," alisema Dkt. Yonazi
=MWISHO=