Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Simbachawene akabidhi Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Uratibu na Udhibiti wa Maafa.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene amekabidhi rasmi mradi wa ujenzi wa Kituo cha Uratibu na Udhibiti wa Maafa kilichopo eneo la Nzuguni “B” Jijini Dodoma kwa mkandarasi Lwanda Limited kutoka Morogoro.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika tarehe 14 Mei, 2022 na kuhudhuriwa na viongozi wa ofisi yake pamoja mshauri elekezi na mkandarasi amewataka kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia umuhimu wa kituo hicho katika kuratibu shughuli za maafa nchini.

Aliongezea kuwa, tayari fedha zimeshatolewa kiasi cha shilingi bilioni 2.442 ambazo zitatumika kuhakikisha ujenzi unaanza haraka bila kukwama.

“Kipekee nimpongeze Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha kuhakikisha ujenzi unaanza ili kuendelea kuratibu masuala ya maafa kwa ufanishi mkubwa hivyo ipo haja ya kuifanya kazi hii kwa weledi na kuikamilisha kwa wakati,”

Uwepo wa kituo utasaidia kuongeza hali ya usalama katika anga, nchi kavu na kwenye maji kwa kuzingatia jitihada za serikali katika kuhakikisha usalama wa wananchi ili kuendelea kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kwa utulivu.

Akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Michael Mumanga alisema mradi umetengewa eneo la  ukubwa wa ekari 106 hivyo kituo kinatarajiwa kuwa kikubwa chenye kukidhi mahitaji yaliyopo nchini ili kutoa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.

“Muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 12 baada ya makabidhiano ya eneo la kazi na kazi zitaanza rasmi tarehe 30 Mei, 2022 na tunatarajia mkandarasi aukabidhi mradi huu tarehe 29 Mei, 2023,”alieleza Meja Jenerali Mumanga

=MWISHO=