Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Pindi atoa maagizo kwa wadau wa Chaneli ya Utalii Tanzania


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe.  Balozi. Dkt. Pindi Chana amewataka wadau wa chaneli ya utalii Tanzania Safari, kuhakikisha wanatanua wigo wa vipindi vya utalii viweze kuonekana katika mitandao ya kijamii. 

Waziri Dkt. Pindi alitoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akizungumza na wadau wa chaneli hiyo na Manaibu Mawaziri kwa lengo la kujadili mikakati na  maboresho ya channeli  ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake.

Alisema kwamba baada ya uzinduzi wa Chaneli hiyo  uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa  Disemba, 2015 iliundwa  kamati ya watendaji wa wizara  kujadili na kutoa mapendekezo yatakayoboresha  uendeshaji wake  kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kimataifa.

“Moja ya mapendekezo ilikuwa ni kuhakikisha inapatikana katika visimbuzi vyote  na majukwaa mengine nchini  na hapa kuna wataalamu mtatuambia  hii haitoshi tuweke na kwenye simu, mitandao ya kijamii  ndiyo maana kikao cha leo kina wabobezi hivyo ni lazima tufikiri nje ya boksi  kama tunazungumzia utalii siyo lazima mtu afike nyumbani ndipo awashe luninga yake zionekane hata katika vyombo vya usafiri,”alisema Mhe. Pindi.

Kuhusu athahari ya UVIKO -19 katika sekta ya utalii Mhe. Pindi alisema pato linalotokana na utalii lilishuka kutoka dola za Kimarekani Bilioni 2.532 mwaka 2019 hadi Bilioni 1.107 mwaka 2021 lakini bado inatajwa kama sekta muhimu kwa uchumi wa Nchi.

Hata hivyo Waziri Pindi alibainisha  kwamba chaneli hiyo inapaswa kuwa endelevu na vipindi vinavyoandaliwa  viwe vyenye  ushawishi kwa wananchi kuvutiwa kutembelea vivutio vilivyopo nchini hata mataifa ya nje kutembelea vivutio hivyo.

“Vivile  kikao hiki kitoe mapendekezo ya namna ya kupata fedha za dharula kwa jili ya kushughulikia uandaaji wa vipindi vipya na kuweka mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa chaneli hii  na kamati ya Mheshimwa Waziri Mkuu ilikutana Disemba 27, 2018 kuweka mikakati ya uendelevu wa chaneli ikiwemo ubora unaozingatia viwango vya kimataifa, uhitaji wa mafunzo, upatikanaji wa vifaa vya kisasa na kuwezesha chaneli kupatikana  katika majukwaa yote,”alisisitiza Mhe. Pindi.

Alihitimisha kwa kusema masuala ya utalii ni mtambuka yanayoshirikisha sekta mbalimbali kama sekta ya utalii, sekta ya uchukuzi, sekta ya habari na mawasiliano na  sekta ya fedha hivyo kama wasimamizi wa sera katika Wizara husika ipo haja ya kuifahamu chaneli hiyo, lengo la kuanzishwa na umuhimu wake kwa sekta ya utaliii na uchumi kwa Nchi.

Akieleza mapendekezo yaliyofikiwa na wataalamu wa sekta hiyo mara baada ya kikao Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya alieleza maazimio yaliyofikiwa kwamba ni pamoja na Mawaziri kuendelea kupewa nafasi ya kuwasilisha mawazo yao, wanaochangia kwa kujitolea kuwezesha chaneli watambuliwe  na kila taasisi kuweka utaratibu utakaowezesha uchangiaji wa Safari Chaneli.

Aidha Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji (TBC) Dkt. Ayoub Ryoba akaeleza mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa chaneli hiyo ambayo ni ununuzi na ufungaji wa mitambo ya kidigitali, kurusha matangazo kote Duniani, kurushwa vipindi vyake kupitia visimbuzi vyote nchini, kuboresha vifaa, kutoa elimu ya utalii kwa watanzania kuptia vivutio vya kiutamaduni, hifadhi za wanyama na utalii wa Ikolojia.

=MWISHO =