Habari
Waziri Mkuu atoa maagizo kumi yatakayoboresha sekta ya sheria nchini.
Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa ametoa maelekezo kumi yanayohusu masuala ya sheria nchini kwa lengo la kuboresha sekta hiyo na kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora ya sheria kwa viwango vinavyotakiwa kiutumishi na kitaaluma pamoja na kukidhi matarajio ya kuufikia ustawi wa jamii na nchi kwa ujumla.
Amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania leo tarehe 21 Machi, 2024 Jijini Dodoma.
“Sasa nitumie nafasi hii kutoa msisitizo katika masuala muhimu yafuatayo
Maafisa Sheria pamoja na Mawakili wa Serikali wote nchini tekelezeni majukumu yenu ya kisheria kwa uadilifu, weledi, uwajibikaji, uaminifu, usiri, umakini na kwa kujituma. Pia, Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali nchini kote shirikianeni kikamilifu katika kutekeleza Kampeni ya utoaji msaada wa kisheria ya Mama Samia. Hakikisheni kuwa kampeni hii inapewa uzito kama mojawapo wa majukumu yenu mahsusi”, amesema Mhe. Waziri Mkuu.
Maagizo mengine aliyoyatoa ni pamoja na Uongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na watoa huduma wengine kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inatolewa kwa wananchi wote wenye uhitaji bila ubaguzi wa namna yoyote.
Aidha, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Taasisi nyingine za utoaji haki wafungue na kuimarisha ofisi zao katika ngazi za chini ili kuhakikisha huduma za kisheria zinafika kwa wananchi wote kwa wakati na bila usumbufu.
Mhe. Waziri Mkuu ameitaka TAMISEMI iratibu Kamati za Mikoa za Kuratibu Huduma za Msaada wa Kisheria ambazo nyingi kwa sasa hazifanyi kazi, ziwezeshwe kifedha na kinyenzo ili ziweze kuwahudumia wananchi katika mikoa yao kwa tija na wepesi.
Vilevile, amesisitiza Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuweka mipango ya kutafuta vyanzo vya fedha ili kuwezesha kamati za mikoa kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Pamoja na kushirikiana na wadau wake wa sheria, kuhakikisha kuwa watoa huduma wote bila kujalisha maeneo walipo wanawezeshwa fedha na nyenzo za kazi pamoja na kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili yawasaidie katika kutekeleza majukumu yao.
“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iwezeshe upatikanaji wa nakala za Miongozo iliyotokana na sheria zote zilizofanyiwa urekebu na ufasiri ili kusaidia watoa huduma za msaada wa kisheria na wananchi kuzielewa na kuzitumia. Wananchi watumie fursa ya uwepo wa tafsiri za sheria kwa lugha ya Kiswahili ili kufahamu haki zao.
"Ninawapongeza sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi ya ufasiri wa sheria za nchi kwa lugha ya Kiswahili”, amesisitiza Mhe. Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu ameongeza “Mawakili wote wa Serikali wajisajili kwenye mfumo wa OAG-MIS. Hii itawawezesha wananchi kuwajua mahali walipo pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za sheria mbalimbali kwa urahisi na mahitaji makubwa ya wananchi upande wa huduma za sheria yanahusiana na upatikanaji wa elimu katika utatuzi wa migogoro katika maeneo ya makosa ya jinai, ndoa, ardhi, kazi na mirathi. Hivyo basi, wekeni mkakati mahususi wa kuendelea kuelimisha wananchi katika maeneo hayo”.
Katika hatua nyingine, Mhe. Waziri Mkuu amesema kuwa anatambua jitihada zinazofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Pia amezipongeza asasi za kiraia, taasisi za umma na binafsi kama Chama cha Wanasheria Tanganyika, Legal and Human Rights Centre (LHRC), Tanzania Legal Aid Providers (TANLAP), Legal Service Facility (LSF), Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC).
“Vilevile, ninatambua mchango mkubwa wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria, UNDP, UN Women, Polisi, Magereza na makundi mengine yote katika kutoa huduma za kisheria. Niwahakikishie kwamba Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa wadau wote wa utoaji huduma za kisheria.
Aidha Serikali itaendelea kutoa rasilimali muhimu ili kuziwezesha taasisi zinazotoa huduma za kisheria kutoa huduma kwa ufanisi. Kundi hili kubwa la Maafisa Sheria na Mawakili wa Serikali limebeba dhamana kubwa ya kutoa huduma za kisheria.
"....nendeni mkaitendee haki dhamana hii kubwa kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania”. Ameeleza Mhe. Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mheshimiwa Jaji Dkt. Eliezer Feleshi akieleza lengo la mkutano huo amesema Mkutano ni jukwaa la kitaaluma la wansaheria wa umma, lengo kutoa fursa kwao kujadili maendeleo ya sekta ya sheria kwa ujumla ambao hufanyika mara moja kwa mwaka, ukiwa na lengo la kukuza ufanisi wa wanachama, kujenga uelewa kuhusu maendeleo ya huduma za kisheria na kutoa fursa kuwawezesha kutathmini mafanikio na changamoto wanazokutana nazo katika taasisi zao na mafunzo yanayowakabili katika kutoa huduma za kisheria.
“Ofisi yangu itaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuwezesha kuyafikia matarajio ya chama hiki,” alisema Jaji Dkt. Feleshi
Akizungumzia Kaulimbiu ya mwaka huu amesema inawakumbusha kuendelea kutekeleza majukumu ya kuhudumia wananchi kwa weledi na ustadi ili kuendelea kuwa na amani na kuchochea ustawi wa jamii yetu ili kuimarisha misingi ya haki na usawa.
“Mawakili wa Serikali tutaendelea kutumia mifumo na miongozo katika kuhudumia wananchi wote nchini.Kila mmoja ana wajibika kuweka mikakati madhubuti katika kuitekeleza kauli mbiu hii kwa weledi, hasa kuwafikia wananchi wasio na uwezo,”.