Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu atoa agizo kwa mkarandasi anayejengwa barabara ya Nanganga-Ruangwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya China inayojenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga na kuwataka waongeze kasi ili waweze kukamilisha kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Julai 26, 2021) alipokutana na viongozi hao katika kijiji cha Namahema  wilayani Ruangwa. Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 53.2 inatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bilioni 59.28 na imepangwa kukamilika Novemba 2022.

Mheshimiwa Majaliwa amesema barabara ya Ruangwa - Nanganga ni muhimu kwani kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo yakiwemo mazao mbalimbali ya kilimo hivyo kuchangia katika kukuza uchumi na kuongeza tija kwa wakulima.

Kwa upande wake, Meneja Mkaazi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation Bi Su Jinlan amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wataongeza kasi ya ujenzi wa mradi wa barabara hiyo na kwamba itakamilika kwa wakati. Hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 18 ya utekelezaji.

Meneja huyo amesema kuwa kampuni yao imejipanga ipasavyo na wanatarajia kuongeza vifaa vya kufanyia kazi ili waweze kukamilisha ujenzi mradi kama ilivyokusudiwa. Pia amewashukuru wananchi wa wilaya hiyo kwa ushirikiano wanaoutoa kwao.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Gogovivu wilayani Ruangwa ambapo ametumia fursa hiyo kuwasisitiza waendelee kuiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Akizungumzia sekta ya elimu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na mchakato wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea elimu ukiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa. “Leo hii kata zote za wilaya ya Ruangwa zina shule za sekondari.”

-End-