Habari
Waziri Mkuu asisitiza utatuzi wa kero kuanzia ngazi ya kijiji
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema serikali haikuweka ofisi nyingi kwa ajili ya kugawana vyeo bali kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu yao, hivyo amewataka viongozi na watumishi wa umma kushughulikia kero za wananchi kuanzia ngazi za vijiji na kata badala ya kuwaacha wananchi wahangaike kufuatilia huduma hadi ngazi za juu.
Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili Mei 24, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilazimika kusafiri hadi Dodoma kufuatilia huduma na madai yao jambo ambalo linaongeza usumbufu wakati viongozi waliopo kwenye maeneo yao wanapaswa kushughulikia changamoto hizo mapema kupitia mfumo wa kiutendaji uliopo serikalini.
“Hatukutengeneza ofisi nyingi ili tugawane vyeo. Tumetengeneza ofisi nyingi kuwasaidia wananchi kero yao wasiende mbali. Kwa nini mnataka mwananchi yeye mwenyewe aangaike na kero yake mpaka kwa Rais?” alisema Dkt. Mwigulu.
Aidha, Waziri Mkuu alisema serikali itaendelea kusimamia uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa umma ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa haki.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu alisisitiza umuhimu wa viongozi kusimamia haki za wananchi hususan kwenye migogoro ya ardhi na fidia, akionya dhidi ya matumizi mabaya ya madaraka yanayowaumiza wananchi.
“Lazima Watanzania wote wafurahie matunda ya uhuru wa nchi yao. Hakuna mahali panaposema ukishakuwa na mali, ukishakuwa tajiri, wewe ni Mtanzania na nusu na wengine ni nusu Watanzania,” alisema.
Pia aliwataka watendaji wa sekta ya afya kuhakikisha dawa zinazotolewa na serikali zinawafikia wananchi badala ya wagonjwa kuelekezwa kununua dawa katika maduka binafsi wakati serikali imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James alisema Wilaya ya Kilolo ni miongoni mwa wilaya zinazofanya vizuri katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo pamoja na mazao ya misitu huku changamoto kubwa ikiwa ni miundombinu ya barabara.
Naye Mbunge wa Kilolo, Rita Kabati alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo wilayani humo huku akiomba serikali kuharakisha ujenzi wa kilomita 17 zilizobaki kuelekea Dabaga ili kufungua zaidi uchumi wa wananchi wa Kilolo.




