Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu aitaka Bodi ya Korosho kutafuta masoko ya uhakika


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Bodi ya Korosho Tanzania ihakikishe inatafuta masoko ya uhakika ya zao hilo na yatakayotoa bei nzuri na kuwanufaisha wakulima.

Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo isimamie mwenendo wa ujenzi wa viwanda vidogo na vikubwa vya kubangulia korosho katika maeneo yote yanayolima zao hilo ili kuondokana na uuzwaji wa korosho ghafi.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa maagizo hayo leo (Alhamisi, Julai 22, 2021) wakati akizungumza na Wakuu wa mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Ruvuma, Mrajisi wa Ushirika, Viongozi wa vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho katika kikao kilichohusu upatikanaji wa pembejeo za korosho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa mkoani wa Lindi.

Amesema lazima bodi hiyo ambayo ameizindua lazima iwajibike ipasavyo katika kuhakikisha inaongeza uzalishaji wa zao hilo na iwapo itashindwa Serikali haitosita kuivunja. 

"Lazima mfuatilie na kuufahamu mwenendo wa zao mnalolisimamia na mjue mfumo unaotumika katika mauzo yake. Pia muwe na takwimu za wakulima na ukubwa wa mashamba yao ili kuweza kuwahudumia kwa urahisi."

Waziri Mkuu amesema bodi hiyo inatakiwa iandae kalenda maalumu inayoonesha hatua zote zinazopaswa kufuatwa katika kilimo cha zao hilo kuanzia hatua za uandaaji wa shamba hadi mavuno kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika na ipelekwe kwa wakulima.

Amesisiza kwamba utaalamu lazima ufuatwe na uzingatiwe katika kilimo hilo kwa lengo la kuongeza tija kwa wakulima. Pia, Waziri Mkuu ameitaka bodi hiyo ihakikishe pembejeo ikiwemo miche bora na viuatilifu vinapatikana kwa urahisi.

Kadhalika, Waziri Mkuu ameigiza bodi ya korosho iweke mkakati wa utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na faida ya kulima zao la korosho. "Tumieni magari maalumu kwa ajili ya kwenda kuwafuata wakulima katika maeneo yao na kuwapa elimu."

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema tayari mchakato wa kuviwezesha vyama vya wakulima kuanza ubanguaji wa korosho umeanza ambapo katika msimu wa mwaka huu TANECU imepata mkopo kutoka CRDB na itaanza kubangua tani 2,500.

Amesema vyama vingine vitakavyofuata utaratibu huo baada ya TANECU ni TAMCU, MAMCU na RUNALI ambavyo vyote vinampango wa kuanzisha viwanda vyenye uwezo wa kuchakata tani 2,5000 za korosho kwa mwaka.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho, Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema wamepokea maelekezo na maagizo yote kwamba watayafanyia kazi kwa kusirikiana na wajumbe wa bodi hiyo na Menejimenti na kwamba hawatafanyakazi kwa mazoea.

-End-