Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mkuu aagiza ufuatiliaji miradi ya Serikali


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza ufuatiliaji wa karibu ufanywe kwenye miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mji wa Serikali ili ubora wa miundombinu inayojengwa ulingane na thamani halisi ya fedha iliyotumika.

“Taasisi za umma zikamilishe ujenzi wa majengo yao hapa Dodoma ili yaanze kutumika. Ninafahamu kuwa upo utaratibu wa kuhamishia Taasisi na Wakala za Serikali hapa Makao Makuu ya Serikali, kila taasisi izingatie utaratibu uliowekwa.” 

Alitoa maagizo hayo jana Jumanne, Februari 6, 2024 alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika haflla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi ya Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo (WMA) katika eneo la Medeli jijini Dodoma.

Waziri Mkuu alisema ujenzi wa ofisi za taasisi uzingatie ushirikishwaji wa karibu wa taasisi za usimamizi wa miundombinu wezeshi ili kuwa na mfumo bora unaoendana na mpango kabambe  unaolenga kuwa na jiji  linalotekeleza dhana ya Jiji Janja (Smart City).

Akizungumzia kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Mji wa Serikali, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake inaendelea kutekeleza mpango wa kuhamia Dodoma ambapo awamu ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya Ofisi katika mji huo  uliopo Mtumba imekamilika.

Mheshimiwa Majaliwa alisema awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya ofisi za Wizara yatakayotosheleza mahitaji ya watumishi wote unaendelea. Katika awamu hii jumla majengo 29 yanajengwa, kati ya hayo majengo 26 ni ya Ofisi za Wizara, na taasisi ni matatu.

Hadi kufikia Januari mwaka huu hatua ya ujenzi wa majengo yote imefikia wastani wa asilimia 73.4, baadhi ya taasisi zimeshapiga hatua kubwa katika ujenzi huo kama Wizara ya Maliasili na Utalii (99.9%), Wizara ya Maji (99.5%) na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma (94.6%)”.

Alisema mpango huo wa ujenzi wa majengo unatekelezwa sambamba na ujenzi wa miundombinu ya kudumu inayopita chini ya ardhi na kwa kuwa baadhi ya majengo yako katika hatua ya kumalizia, utaratibu wa ununuzi wa samani unaendelea ili yatakapokamilika watumishi wote waweze kuhamia. “Hii itawezesha wananchi kupata huduma muhimu za Serikali katika eneo moja.”

Mheshimiwa Majaliwa alisema jitihada za Serikali ya awamu ya sita inaoyoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kazi na muonekano wa Jiji la Dodoma zinaonekana na miradi mikubwa ya ujenzi inaendelea kutekelezwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato.