Habari
Waziri Mkuu aagiza jedwali la utatuzi wa kero za wananchi
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewaagiza watendaji wa Serikali kuandaa jedwali la kuonesha namna walivyotatua kero za wananchi katika kila wiki ya mwisho wa mwezi.
Amesema hayo leo Jumapili (Machi 01, 2026) katika mkutano wa hadhara uliofanyika Stendi za Zamani, Babati Mjini mkoani Manyara.
Amesema kuwa Serikali haiwezi kukubali utaratibu wa kulimbikiza matatizo ya watu kana kwamba Serikali haipo.
Ameongeza kuwa Serikali imetengeneza utaratibu ndani ya nchi wa kuwa na uongozi katika kila eneo kwa ajili ya kuwarahisishia wananchi kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
“Hatukutengeneza ofisi hizi za Serikali ili kugawana vyeo. Ninawahakikishia tukianza kufuatilia tutajua nani anaweza kazi na anastahili kukaa ofisini.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaangalia upya suala la changamoto ya ardhi nchini.
Amesema haiwezekani kuwepo na migogoro ya ardhi ya muda mrefu ambayo haiishi hadi kufikia hatua ya kutishia undugu miongoni mwa Watanzania.
“Inaanza kutishia Utanzania wetu, kwa hiyo hili jambo la ardhi tutaliangalia upya. Hatuwezi kuwa na jambo ambalo linakuwa sehemu ya maisha yetu. Mungu alitupa akili binadamu kuliko wanyama wengine, haiwezekani kila kona tatizo ni hilo hilo.”




