Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama atoa rai wananchi kuondoka maeneo hatarishi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amewataka  wananchi kuondoka katika maeneo hatarishi  ili kujikinga na mafurikio ya mvua za vuli zinazoendelea kunyesha.

Kauli hiyo ameitoa wakati alipotembelea na kujionea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ya mvua katika Halmashauri  ya Mlimba Mkoani Morogoro ambapo amewaomba wananchi kuendelea kufuatilia na kusikiliza ushauri wa serikali.

Waziri Mhagama amewataka wananchi kuendelea kushikamana ili kupambana na majanga ya Mafuriko, ambayo yameleta kadhia kubwa kwa wananchi.

“Serikali imetengeneza Mpango wa Dharura wa kukabiliana na mvua za El Nino na mvua za Masika, ambapo serikali itafanya kila linalowezekana kuzuia madhara yasitokee na hasa maisha ya watanzania,” alisema Waziri Mhagama

Ameongeza kuwa, mafuriko ya maji yamesababisha udongo kumomonyoka na kuharibu miundombinu ya reli na kuleta madhara mengine mengi  hivyo ni vyema kuendelea kusikiliza ushauri wa serikali.

“Serikali itaendelea kuhakikisha inapambana dhidi ya magonjwa ya Mlipuko na uhaba wa chakula  na madhara mengine ambayo yameathiri wananchi, serikali itakuwa pamoja na nyinyi katika kutatua kadhia hizo alibainisha,” alisisitiza Waziri Mhagama

Aidha aliwakumbusha wananchi kuendelea kuliombea Taifa hali iliyopo ili kuendelea kuwa na jamii stahimilivu ya maafa na kuendelea kuishi kwa usalama mkubwa.

Ameeleza kwamba katika utabiri wa hali ya hewa unaoendelea kutolewa unaonesha mvua hizi zinaendelea kunyesha hivyo ni vyema kuendelea kuchukula tahadhari.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kilombero Mhe. Dustan Kyobya amesema changamaoto ya Mawasiliano ya barabara kwa watu wa Masagati na Utengule kwao wamekuwa kisiwa kutokana na miundo mbinu ya barabara kutopitika, lakini pia Mawasiliano kati ya Jimbo la Ifakara na Mlimba ambazo zinatengeneza wilaya ya kilombero nayo ni magumu.

“Nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuma ndege kwa ajili ya kuokoa watu waliokwama na kuruhusu treni ya Mwakyembe  kuanza kubeba abiria ili kurahisisha mawasiliano,” alisema Mhe. Dustan

Awali Bi, Zainabu Makenjula Mkazi wa Mlimba ameomba serikali kushughulikia suala la barabara kwa wakati ili kurahisisha mawasiliano na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji kwa sababu kuna maeneo magari wala pikipiki haviwezi kupita.

=MWISHO=