Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Mpango wa mkoa wa Afya Moja waandaliwa Tanga


MPANGO wa Afya Moja kwa mkoa wa Tanga umeendelea kuandaliwa ukiwa na lengo la kuainisha Afua mbalimbali za kuboresha uratibu wa utekelezaji wa Dhana ya Afya ya Moja.

Timu ya wataalam kutoka sekta za afya, mifugo, mazingira, wanyamapori na kilimo imekutana katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga kwa siku Tano kuanzia Aprili 13 hadi 17, 2026 ili kuandaa Mpango huo utakaotumika kubaini rasilimali zitakazosaidia kutatua changamoto na vihatarishi vya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Maandalizi hayo yameratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Sehemu ya Afya Moja kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani ili kuona namna bora ya kuwaleta wadau wa masuala hayo ili kuhakikisha wanaleta tija katika kuuandaa mpango huo kwa mkoa wa Tanga.

Ikumbukwe kuwa, Dhana ya Afya Moja imeendelea kupigiwa chapua kwa kuzingatia umuhimu wake kwa jamii nzima na ambayo hujikita katika kujumuisha sekta zote za Afya katika kujiandaa, kufuatilia  na kukabili magonjwa yanayomuathiri binadamu imeendelea kufundishwa kwa Wataalamu wa sekta hizo za Afya, ikiwa ni Sekta ya Afya  ya Binadamu, Wanyamapori, Mifugo, Kilimo na Mazingira, ili wataalamu hao watumie dhana hiyo kuimarisha udhibiti wa magonjwa ambukizi kati ya Binadamu na wanyama  ambayo hutokea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ikiwemo yale ya mipakani kutokana na kuwepo kwa  mwingiliano mkubwa kati ya  watu na wanyama katika mazingira yao.

Hivyo, dhana ya Afya Moja (One Health) inatoa fursa ya kutambua uhusiano wa karibu kati ya afya ya binadamu, wanyama, na mazingira, ikilenga kuzuia magonjwa ya mlipuko kama Zoonotiki hivyo sekta zikiungana pamoja itaimarisha udhibiti wa magonjwa na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na afya jamii na kulinda ustawi wa viumbe vyote.

 

=MWISHO=