Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Waziri Mhagama awataka wakandarasi ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba kuongeza kasi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, amewataka wakandarasi wanaondelea ya shughuli ya ujenzi wa majengo ya Mji wa Serikali Mtumba Dodoma kuongeza kasi, na kufanya vikao vya mara kwa mara ili kuweza kutatua changamoto za ujenzi wanazokutana nazo.

Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Mei 6, 2023 alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa baadhi ya majengo hayo na kuwaasa wakandarasi hao kujenga majengo yanayoendana na thamani ya fedha zilizopangwa na kuhepuka ucheleweshwaji ili kufikia malengo ya Serikali.

“Fanyeni kazi kwa pamoja na kuhakikisha mnaongeza kasi ya ujenzi, muwe na site meetings, tatueni changamoto kwa wakati, thamani ya fedha ilingane na mradi na thamani ya mradi iendane na fedha, hatuhitaji kuwa na delays yoyote katika ujenzi wa mradi huu,”alisema Mhe. Mhagama

Alipokuwa katika Jengo la Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, aliwaasa Wakandarasi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kutumia fursa ya ujenzi wa Mji wa Serikali  kwa kufanya kazi kwa weledi ili kuweza kuuza ujuzi kwa wageni watakaotembelea mji huo  wa Serikali mbeleni na kuwawezesha kuteka soko la Nchi za Afrika Mashariki na nchi za kusini mwa Afrika.

Kwa Upande wake Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Wizara hiyo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa NHC Mhandisi Aikani Mlekeo Alisema “ Tunaishukuru Ofisi ya waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu chini ya Usimamizi wa mratibu wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Bw. Mesharck Bandawe, kwa kutupa Mwongozo mzuri katika usimamizi wa Ujenzi wa Mradi huu.”

Ziara hiyo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, ilihusisha kutembelea na kukagua baadhi ya ujenzi wa majengo ya Serikali ikiwa ni pamoja  Eneo la ujenzi wa Mradi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu na Eneo linalojengwa Uwanja wa Mashujaa.

 

=MWISHO=