Habari
Waziri Jenista aagiza Mwongoza Lishe kuanza kutumika mwezi Julai, 2021
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge,Uratibu, Kazi,Vijana ,Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameziagiza Taasisi za TFNC, MUHAS, SUA, TBS kuharakisha uandaaji wa mwongozo lishe ili uanze kutumika kuanzia mwezi Julai, 2021
Waziri Mhagama ametoa agizo hilo alipotembelea na kukagua utekelezaji wa mradi wa Boresha Lishe katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma Julai 6,2021
“Jambo hili limeingia kwenye programu ya kwanza ya boresha lishe ninaomba Watanzania wote tushukuru, tuunge mkono na hatuna haja ya kuchelewa tena na Mwongozo huu utoke kabla ya mpango wa pili haujaanza”Aliongeza Waziri Mhagama
Amesema kuwa mwongozo huo utaliondoa Taifa kwenye tatizo la udumavu kwa kiasi kikubwa sana kama kila mtu atajuenga tabia ya kunywa uji wa lishe bora.
“Tujenge tabia ya kunywa kikombe cha lishe kila asubuhi,wafanyakazi wanywe,wanafunzi wanywe,uji huu utabadilisha mtazamo na kuboresha afya za watoto, wakubwa na wazee wote kwani wanaitaji kuwa na lishe bora,mimi mwenyewe nitaongoza kampeni ya kunywa uji wa lishe asubuhi ”Alisisitiza Waziri Mhagama.
Aidha amesema mradi huo umeweza kuongeza wanawake wanaokula vyakula mchanganyiko ambavyo ni vya asili kutoka asilimia 17 mpaka asilimia 49.
Pia idadi ya watoto kutoka miezi 6-23 wanaopata vyakula mchanganyiko imeongezeka kutoka asilimia 3 mpaka 35 na kusisitiza kuwa mradi huu umekuwa na faida kubwa sana.
Mradi wa Boresha Lishe unaoendeshewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani na kufadhiliwa kwa pamoja na Umoja wa Ulaya ukilenga kuimarisha upatikanaji na matumizi ya chakula chenye lishe kwa wanawake na watoto kupitia ya mabadiliko ya tabia, kuzalisha vyakula mchanganyiko na kusambaza chakula bora katika Wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Wilaya za Ikungi na Singida Vijijini Mkoani Singida.
=MWISHO=