Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

“Wanawake jitokezeni kugombea nafasi za uongozi” Mhe. Nderiananga


Serikali kupitia Mjasili wa Vyama vya Siasa imesema ina mkakati  kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha  wanawake wanashiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga  wakati wa Bunge la 12, Mkutano wa 13 Kikao cha Pili wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Anatropia Lwehikila Theonist kwa niaba ya Waziri Mkuu akitaka kufahamu Wanawake wangapi wamekuwa Wabunge wa Majimbo na Madiwani katika chaguzi tatu mfululizo zilizopita.

Mhe. Ummy amesema Serikali inatambua na  kuthamini ushiriki wa wanawake katika siasa hivyo kupitia Ofisi ya Msajili wa vyama siasa  itaendelea kutoa elimu kwa wanawake na makundi mbalimbali kuwajengea uwezo wa kujiamini na kujiandaa kugombea nafasi hizo akisema kundi hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

“Niwatoe hofu wanawake wenzangu Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajali na kuwathamini wanawake na tutaendelea kufanya vizuri kuhakikisha tunawajumuisha wanawake katika ngazi zote za maamuzi. Serikali inatambua ushiriki wa wanawake katika shughuli za kisiasa na meneo mengine na katika eneo hili mkakati uliopo ni kutoa elimu kwa wanawake kujiamini na kuthubutu,”Amesema Mhe. Ummy.

Pia Mhe. Ummy ameongeza kuwa Serikali inatarajia kupeleka mabadiliko ya sheria ya Vyama vya siasa itakayovitaka vyama hivyo kuwa na sera itakayoweka muongozo mahususi wa kujumuisha wanawake kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Aidha amebainisha kwamba  Katika kipindi cha kuanzia 2010 hadi 2020 zilifanyika Chaguzi tatu katika ngazi ya Ubunge na Udiwani ambapo katika chaguzi hizo, jumla ya Wabunge wanawake 73 walishinda chaguzi hizo na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Majimbo huku upande wa Madiwani Jumla ya Wanawake 654 wakichaguliwa kuwa Madiwani katika Kata husika.

=MWISHO=