Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Wajumbe Baraza Kuu Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Waipongeza serikali kwa ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba


Wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, wakiongozwa na Mwenyekiti Fadhili Maganya, wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa mji wa Serikali, Mtumba.

Bw. Maganya ametoa pongezi hizo alipoongoza ujumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa kutembelea Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma.

"Tunaona namna Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais na Mwenyekiti wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ujenzi wa Mji huu wa kisasa ambao sio tuu watu kuja kufanya kazi bali hata kukuza  utalii wa ndani" amesema Bw. Maganya.

Aidha, Bw. Maganya ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara, majengo ya kisasa na matumizi ya samani zilizotengenezwa ndani ya nchi vinaonesha thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali na kuahidi kushirikiana na Serikali katika upandaji wa miti ili kuwa sehemu ya kutimiza malengo ya utunzaji wa mazingira katika mji huo.

 Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) Mheshimiwa Ummy Nderiananga amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU) itaendelea na uratibu wa ujenzi wa mji wa Serikali kwa kiwango kinachohitajika na amewashukuru Jumuiya ya Wazazi Taifa kwa  kutenga muda wa kutembelea Mji wa Serikali ili kujionea kwa macho utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akiwakaribisha Wajumbe hao, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Paul Sangawe amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu inapokea wageni mbalimbali wanaotaka kutembelea Mji wa Serikali Mtumba na kuufanya Mji huo kuwa kivutio cha utalii.