Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Ufuatiliaji na tathmini haviepukiki katika utekelezaji wa miradi na mipango ya maendeleo


Imeelezwa kuwa, Suala la Ufuatiliaji na Tathmini lina umuhimu mkubwa katika kuangalia utekelezaji wa Mipango kuanzia ngazi ya mamlaka za chini hadi ngazi ya taifa katika utendaji hususan kwenye miradi, ikilinganishwa na namna gani inakwenda sawasawa au inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Cosmas Ngangaji katika siku ya pili ya Kongamano la Pili la Wiki ya Kitaifa ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea jijini humo ambapo amesema kuwa Suala Ufuatiliaji na Tathmini linajikita zaidi katika vitendea kazi vinavyotakiwa kutumika pamoja na michakato inayotumika kama inafanya kazi na kuleta matokeo chanya hususan katika sekta ya Umma.

Akitolea mfano wa dhana ya tathmini ya utoaji wa huduma za kijamii, Bw. Ngangaji alisema kuwa, miradi mingi ya Serikali inatakiwa kuwekewa misingi endelevu ili wananchi waweze kupata huduma sahihi na kwa wakati.

Akiongea katika kongamano hilo Bw. Mussa Mshirazi Mbarouk kutoka Tume ya Mipango ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisema, suala la Ufuatilijai na Tathmini ni suala linalohitaji kujifunza mara kwa mara ili kusaidia kujenga uwezo katika utendaji wa shughuli za kila siku.

Kongamano la Pili la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini linaloendelea Jijini Arusha limeingia katika siku ya pili ambapo mada mbalimbali zimeendelea kuwasilishwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uelewa wa Tathmini, majadiliano bayana juu ya matokeo halisi na mbinu muhimu za kuleta mbadiliko.