Habari
Ubunifu Uendelezaji Makao Makuu, Mji wa Serikali Wahitajika- Dkt. Yonazi
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amesisitiza ubunifu katika uendelezaji wa Makao Makuu na Mji Serikali ili kuweza kuvutia watalii wa ndani na nje.
Dkt. Yonazi ametoa msisitizo huo wakati wa ziara yake nchini Malaysia alipotembelea Mji Mkuu wa Utawala wa Malaysia uitwao Putrajaya.
"Ni muhimu wataalam kuzingatia masuala yanayofanya mji wa Serikali kuwa kivutio kwa wananchi na watalii kutoka nje. Masuala hayo ni ubunifu katika majengo, utunzaji wa mazingira na miundombinu na huduma muhimu hasa nyumba za ibada, huduma za fedha na maeneo ya kupumzika" amesema Dkt. Yonazi.
Aidha, Dkt. Yonazi ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za Kimataifa ili kubadilishana uzoefu na kujifuza masuala ambayo yataongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla.
Katika ziara hiyo Dkt. Yonazi ameambata na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Mhe. Dkt. Mahadhi Maalim, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali Bw. Paul Sangawe, Wataalam kutoka Ubalozi wa Tanzania Nchini Malaysia na kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.