Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tanzania na Qatar wajadili fursa za uwekezaji


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amekutana na Makamu wa Kwanza wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Qatar (QCCI), Bw. Mohammed bin Ahmed bin Twar Al Kuwari na ujumbe wake kwenye kikao kilichofanyika leo Jumapili, Septemba 27, 2026 katika hoteli ya Kempinski, jijini Doha, Qatar. 

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihimiza umuhimu wa kuishirikisha sekta binafsi kwenye mipango ya maendeleo ya nchi kupitia dira 2050 inayotaka uchumi wa Taifa ufikie thamani ya dola za Marekani trilioni moja.

 "Tunaamini kwamba Serikali peke yake haiwezi kufanikiwa katika uwekezaji huo bila kushirikisha wawekezaji wa ndani au wa nje ndiyo maana imeweka vivutio vya kiuwekezaji ili kuvutia mitaji."

Katika kikao hicho, wamejadiliana masuala ya kiuchumi na uwekezaji na kuainisha fursa zilizopo kwenye nchi zote mbili ikiwemo jumuiya za kikanda kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Baraza la Ushirikiano la Nchi za Kiarabu za Ghuba (GCC).

Aidha, kikao hicho kimekubaliana kuhusu umuhimu wa kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka Tanzania na Qatar kupitia taasisi zao za uwakilishi, zikiwemo QCCI, TPSF na TCCIA, kwa lengo la kujadili kwa kina maeneo ya ushirikiano wa kimkakati, biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda cha Qatar (QCCI) alikiri kwamba Tanzania ni eneo muhimu la uwekezaji kutokana na enep lake la kijiografia na rasilimali ilizonazo.

Alisema wafanyabiashara wengi wa Qatar wako tayari kuwekeza lakini wanahitaji elimu zaidi na kujuana na wafanyabiashara wenzao. “Tunaweza kufanya kwa warsha maalum na mikutano ya mtandaoni itakayozikutanisha sekta binafsi za nchi zote mbili. Lengo kuu ni kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo, viwango vya ubora vinavyohitajika, na kuondoa vikwazo vya kibiashara. Milango yetu iko wazi kwa ajili ya ushirikiano na Tanzania,” alisema.

Kikao hicho pia kiliwashirikisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Maghembe; Katibu Mkuu (OR-Mipango na Uwekezaji); Wabunge na watendaji wengine wa Serikali.