Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Tanzania ina umeme wa kutosha – Dkt. Biteko


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Tanzania  ina umeme wa kutosha baada ya kukamilika kwa  Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP ) ambao pekee  unazalisha Megawati 2115.

Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua ya miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II Jijini Dar es Salaam.

Amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na TANESCO baadhi ya maeneo yalikabiliwa changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.

 Dkt. Biteko amefafanua kuwa   upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu na TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme  katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000.

‘’Nataka niseme  mbele yenu ndugu zangu, Mhe. Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote  yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata  Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika,’’ alisema Dkt Biteko.

Aidha, Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza TANESCO kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.

‘’Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto  za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ alisisitiza Dkt. Biteko.

Vilevile, Dkt. Biteko ametembelea Kituo cha Kupokea Gesi Asilia Kinyerezi kwa ajili ya kukagua miundombinu ya kusafirisha gesi na kuwataka kuongeza uzalishaji wa gesi ili kusaidia kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko  aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya nishati  Mha. Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo na  Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange.

Mwisho