Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Taasisi za dini endeleeni kuiunga mkono Serikali-Majaliwa


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa taasisi za dini nchini kuendelea kuiunga mkono Serikali katika utoaji wa huduma za jamii hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali imewekeza katika miundombinu bora ya afya, elimu na maji.

Amesema kuwa kwa upande wake Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, nafuu na kwa wakati katika maeneo yao.

Amesema hayo leo (Jumapili, Novemba 06, 2022) wakati wa ibada maalum ya kusimikwa kwa askofu mteule wa kanisa la baptist Tanzania Askofu Arnold Manase Mollel na viongozi waandamizi katika viwanja vya seminari vilivyopo Ngaramtoni, Arusha 

“Ninapenda niwahakikishie kwamba Serikali kwa upande wake imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu, afya na maji katika kuhakikisha watanzania wote bila kujali dini zao, rangi zao au itikadi zao wanahudumiwa ipasavyo”

Akitolea mfano katika sekta ya afya, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeongeza fedha za kusomesha wataalamu bingwa na bobezi katika sekta ya afya hadi kufikia shilingi bilioni 8 kutoka shilingi bilioni 3 za mwaka wa fedha 2021/2022. “Hii itasaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza rufaa za nje ya nchi”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amezipongeza Taasisi za dini ikiwemo kanisa la Wabaptist wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwaongoza watu na kutatua shida zao za kijamii, kuwapa mafundisho ya kiroho, kutoa ushauri na kuwajenga kiimani. 

“Kwa mfano, katika jumla ya shule za Msingi 19,261 zilizopo nchini, sekta binafsi na taasisi za dini zinamiliki shule zipatazo 2,080. Kwa upande wa Shule za Sekondari 5,540, shule 1,329 ni za Sekta Binafsi na Taasisi za Dini”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amempongeza Baba askofu Anorld Manase Mollel kwa kusimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Wabaptist. “Kusimikwa kwako leo ni ishara ya wazi kuwa waumini wa Kanisa la Wabaptist Tanzania wanayo imani kubwa na wewe na ndiyo maana wamekupa nafasi hiyo ili uweze kusimamia maono na malengo ya ya Wabaptist wa Tanzania”