Habari
Serikali yatangaza fursa za uwekezaji wa utalii wa mikutano katika Mji wa Serikali Mtumba
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) imetangaza rasmi fursa za uwekezaji katika Mji wa Serikali Mtumba, hususan katika sekta ya utalii wa mikutano, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza shughuli za kiuchumi katika Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.
Tangazo hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Bw. Paul Sangawe, wakati wa mazungumzo rasmi na Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Bi. Christine Mwakatobe yaliyofanyika leo Jijini Arusha.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Sangawe ameeleza kuwa Serikali imetenga maeneo maalum katika Mji wa Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Kimataifa cha Mikutano, hoteli za kisasa, na maeneo ya huduma za kifedha, biashara na burudani. Amesisitiza kuwa uboreshaji wa miundombinu mikubwa kama reli ya kisasa (SGR) na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato ni miongoni mwa sababu kuu zitakazochochea mahitaji ya huduma hizo.
“Kituo hiki kitasaidia kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi, na pia kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa cha mikutano ya kikanda na kimataifa,” alisema Bw. Sangawe.
Kwa upande wake, Bi. Mwakatobe ameahidi AICC kuipa Dodoma kipaumbele katika uwekezaji, na kueleza kuwa taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vya kimataifa.
Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa pia kuambatana na maeneo ya maonesho ya biashara, hoteli za nyota tano, maduka, ofisi na maeneo ya kupumzikia, hatua inayolenga kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya Mji wa Serikali.