Habari
Dkt. Mwigulu amwakilisha Rais Dkt. Samia katika mkutano wa 43 wa AUDA-NEPAD
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa 43 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD) uliofanyika kwa njia ya Mtandao, Ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema kuwa Tanzania inaendelea kujidhatiti katika kutekeleza Ajenda 2063 kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu, kilimo na maendeleo ya rasilimali watu.
“Miongoni mwa miradi muhimu ni Mradi wa Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, ambao utazalisha megawati 2,115 za umeme pamoja na mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaounganisha Tanzania na Burundi pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ili kuimarisha muunganisho wa kikanda”
Dkt. Mwigulu amesema kuwa Tanzania inaamini kuwa Afrika inaweza kuwa mahali bora zaidi pa kuishi kwa vizazi vya sasa na vijavyo, endapo kila mmoja atajitoa kikamilifu kulinda na kuhifadhi mazingira kwa njia endelevu.
“Ili kufanikisha malengo yetu ya maendeleo ni lazima tuimarishe ukusanyaji wa mapato ya ndani, kupambana na fedha haramu na kutumia ipasavyo utajiri mkubwa wa rasilimali za asili barani Afrika ili kufadhili Ajenda 2063 kwa ufanisi.
Katika mkutano huo Rais wa Misri Mheshimiwa Abdel Fattah El-Sisi amemaliza muda wake kama mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali ya AUDA-NEPAD na amekabidhi mamlaka hayo kwa Rais wa Angola, Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço.
Baadhi ya nchi zilizoshiriki mkutano huo ni Misri, Tanzania, Angola, Libya, Afrika Kusini, Ghana, Zimbabwe. Aidha katika mkutano huo, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Sidi Ould Tah pamoja na Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Afreximbank Dkt. George Elombi walishiriki.




