Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali yasisitiza ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika maendeleo


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu imeendelea kusisitiza umuhimu wa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta zote za maendeleo kupitia utekelezaji wa sera, sheria, miongozo na mikataba mbalimbali inayolenga kuhakikisha haki na usawa vinapatikana kwa kila mwananchi bila ubaguzi.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Dkt. Jim Yonazi, wakati wa ufunguzi wa kikao cha kujadili ujumuishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu kilichofanyika Mei 26, 2026 jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU), Dkt. James Kilabuko, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Amesema, Serikali inaendelea kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, fursa sawa na huduma bora kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004, Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (CRPD) pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali inayolenga kuondoa vikwazo vinavyozuia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika shughuli kijamii, kichumi na kisiasa.

Dkt. Kilabuko amesema pamoja na jitihada hizo bado kuna changamoto mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo kuhusu ujumuishwaji, ukosefu wa huduma jumuishi katika baadhi ya sekta na changamoto za utekelezaji wa sera na sheria katika ngazi mbalimbali, huku akihimiza ushirikiano wa wadau wote katika kuondoa changamoto hizo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Kizito Wambura, amesema kikao hicho kinalenga kuwakutanisha wadau wa utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu ili kujadili namna bora ya kuboresha huduma hizo kwa kuzingatia misingi ya ujumuishwaji.

Naye Meneja wa Programu wa Shirika la Sight Savers Tanzania, Bw. Edwin Maleko, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu, akiahidi kuwa mashirika hayo yataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika jamii kupitia programu mbalimbali za ujumuishaji.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa utoaji na utekelezaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu kutoka taasisi tofauti nchini.

 

=MWISHO=