Habari
Serikali yaendelea kuimarisha uwezo wa kukabiliana na maafa nchini
SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuimarisha uwezo wa nchi katika kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa kutoa mafunzo kwa Timu ya Taifa ya Kukabiliana na Dharura, inayolenga kuongeza ufanisi wa uratibu na utekelezaji wa hatua za kukabiliana na matukio ya dharura.
Hayo yamezungumzwa leo, na Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maudhui ya Ndani kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bw. Condrad Millinga akifungua mafunzo ya siku mbili, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi .
Bw. Milinga amesema, mafunzo kwa timu hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa nchini, hususan katika kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa, taarifa sahihi zinapatikana na tathmini za madhara zinafanyika kwa wakati ili kuokoa maisha, kulinda mali na kupunguza athari kwa jamii.
“Timu hii ina majukumu mbalimbali, yakiwemo kushiriki katika operesheni za kukabiliana na maafa, kufanya tathmini za awali ili kubaini hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa pamoja na kushauri kuhusu mahitaji ya ziada ya rasilimali pale inapohitajika” amesema Bw. Milinga.
Aidha, ameitaka timu hiyo kushiriki katika tathmini za kina za uharibifu na mahitaji yanayotokana na maafa ili kubaini mahitaji ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwa maeneo yaliyoathirika.
Hata hivyo ameendelea kusema, majukumu mengine ni kutoa ushauri kwa Kamati ya Wataalam ya Kitaifa ya Usimamizi wa Maafa kuhusu mikakati bora ya kukabiliana na maafa, kuunganisha kongani za kukabiliana na maafa na kushiriki katika mafunzo mbalimbali yanayolenga kuongeza ujuzi na uwezo wa wadau wa kukabiliana na dharura.
Aidha timu hiyo, itashiriki katika kutafuta rasilimali muhimu kwa ajili ya operesheni za dharura na kushirikiana na Idara husika katika kuandaa mipango ya kukabiliana na matukio ya dharura yanapotokea.
Amefafanua kuwa, hatua hiyo italenga kuimarisha utayari wa nchi katika kukabiliana na maafa kwa kuhakikisha kuwa maamuzi yanayofanywa yanazingatia taarifa sahihi, tathmini za kitaalam na mahitaji halisi ya maeneo yaliyoathirika.
Pia amewasisistiza wajumbe wa Timu ya Taifa ya Kukabiliana na Dharura kufanya kazi kwa ukaribu na Idara ya Menejimenti ya Maafa, chini ya uratibu wa Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa wa ofisi hiyo Brg. Jen. Hosea Ndagala amesema, Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea wajumbe wa timu uelewa wa pamoja, taratibu za utendaji na namna ya kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao.
Ameongeza kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji kati ya wajumbe wa Timu ya Taifa ya Kukabiliana na Dharura na Idara ya Menejimenti ya Maafa ili kuhakikisha kuwa taarifa, tathmini na hatua zinazohitajika wakati wa dharura vinapangwa na kuratibiwa kwa ufanisi.




