Habari
Serikali yaahidi kuendelea kukuza uchumi wa Wananchi
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mkakati wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, hivyo kila Mtanzania afanye kazi kwa bidii.
“Sasa tunakwenda kusimamia maboresho ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, Watanzania wote kila mmoja katika eneo migodini, viwandani, wavuzi, wakulima, wasomi na wafanyabiashara wafanye kazi kwa bidii ili kujiongzea tija.”
Ameyasema hayo jana (Jumapili, Septemba 19, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichopo wilayani Karagwe, Kagera akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Rais Mheshimiwa Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika kila halmashauri. Vyuo hivyo vinatoa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha vijana hao kujiari au kuajiriwa.
Amesema mafunzo hayo ambayo yatakuwa yanatolewa katika taaluma za TEHAMA, ufundi umeme, makenika, ushonaji nguo, utawawezesha vijana wa Kitanzania kujiari au kuajiriwa. “Hatua hii itawakwamua kiuchumi na kuwaondoa katika utegemezi, huu ndio mkakati wa Rais Mheshimiwa Samia.”
Hata hivyo, Mheshimiwa Majaliwa ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao unagharimu shilingi bilioni sita na kumuagiza mkandarasi anayenga ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania ahakikishe anaukamilisha kwa wakati ili malengo ya Serikali yaweze kutimia.
Mradi huo unahusisha ukarabati majengo matano na kujenga majengo mapya manane ambayo ni kubadilisha jengo la utawala kuwa madarasa, kukarabati karakana ya ushonaji, kubadilisha jengo la bohari na kuwa karakana ya ufundi wa zana za kilimo na ufundi bomba.
Pia, kubadilisha bohari ya vitu vya jumla (general store) kuwa karakana ya uchomeleaji na uungaji vyuma (welding and fabrication), kukarabati karakana ya ufundi wa magari (Motor Vehicle Mechanics Workshop).
Majengo yanayojengwa ni jengo la Utawala lenye Maktaba, Maabara ya “electronics” na Maabara ya Kompyuta, jengo la maliwato, jengo la Mafunzo ya ufundi mchanganyiko, jengo la bohari, jiko na bwalo la chakula, karakana ya ufundi umeme na hosteli ya wavulana.
-End-