Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali kusimamia sera zinazohusu lishe Nchini


Serikali imesema itaendelea kuratibu na kusimamia sera zinazohusu masuala ya lishe kama hatua ya kukabiliana na utapiamlo na udumavu ndani ya jamii kuhakikisha inakuwa salama na yenye afya bora.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu  Bw. Eleuter Kihwele mara baada ya  semina  ya kuijengea uelewa Menejimenti ya Ofisi hiyo kuhusu Utekelezaji wa Mpango wa Pili Jumuishi wa Masuala ya Lishe nchini  iliyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Machi 31, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Mkurugenzi huyo alisema kulingana na Mpango wa Taifa wa Lishe wa miaka mitano umesisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi kushiriki katika hatua zote za kupanga na kutekeleza mipango inayohusiana na lishe pamoja na ushirikishwaji wa wananchi.

“Lishe ni suala mtambuka linalohusisha wadau wote na wananchi hasa katika muktadha mzima wa kubadili tabia ya ulaji wa vyakula unaozingatia misingi ya lishe kuwe na nyaraka hizi za mpango wa miaka mitano ambazo zitakuwa ni rahisi kueleweka kwa wananchi  na kutekeleza. Pia ni lazima tuimarishe uratibu na ugharamiaji wa utekelezaji wa mpango ili yote  yatekelezwe kikamilifu ifikapo 2025/2026,” alisema Mkurugenzi huyo.

Pia aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kuratibu shughuli za lishe nchini kwa kuzingatia kuwa kama nchi imeandaa mpango wa miaka mitano wa kuratibu masuala ya lishe baada ya kumalizika kwa mpango wa kwanza wa masuala hayo ambao umetekelezwa kwa miaka mitano.

“Mkutano huu umekuwa na manufaa makubwa kwa washiriki na wadau waliohudhuria kufahamu ni wadau gani wanaopasawa kusimamia masuala haya hivyo imekuwa ni fursa muhimu kwa Menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya uongozi na wakuu wa Idara ambao wanasamamia masuala haya kuelewa na kwenda kusimamia utekelezaji wake,” alieleza Bw. Kihwele.

Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bw. Luitfrid Peter akiwasilisha taarifa ya hali ya lishe nchini alibainisha kwamba wanawake milioni 3.3 kuanzia umri wa miaka 15 hadi 49 wanakabiliwa na uzio uliokithiri na upungufu wa damu ukitajwa kuwa changamoto kubwa.

“Kwenye Nchi za Afrika Mashariki kiwango cha udumavu ni asilimia 31. 8 wakati Shirika la Afya Duniani linapendekeza kiwango cha udumavu kiwe angalau chini ya asilimia 20 kwahiyo bado tuna kazi kubwa ya kuvuta hiyo namba iwe chini ya asilimia hizo na kulifikia hili ni lazima tushirikiane pamoja na wananchi ambao ndiyo walengwa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na afya bora,”alileleza Mtafiti huyo.

Aidha Kaimu Mkurugenzi Sera na Mipango kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Bw. Geoffrey Chiduo alibainisha kwamba mikoa 15 inaongoza kwa udumavu yenye zaidi ya asimia 30 na mikoa 7 ambayo ina zaidi ya asilimia 40 ya watoto ambapo kati ya watoto 10 watoto wanne wana udumavu waka huo ikitajwa kuwa na kiwango kikubwa cha uzalishaji wa chakula na uchumi mzuri.

“Tatizo linaweza kuwa siyo uzalishaji wa chakula ila  ni kuhusiana  uelewa wa  masuala ya lishe bora na zipo sababu nyingi kwanza aina ya chakula wanacholishwa hao watoto hakina mchanganyiko unaotakiwa, hawali kwa wakati na hawali milo inayotosheleza, kukosa matunzo mazuri, uelewa wa waangalizi wa watoto wakiwemo  wazazi na walezi kuhusu lishe bora,” alihitimisha Bw. Peter.

=MWISHO=