Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Serikali kujenga kituo jumuishi cha Parachichi Rungwe


SERIKALI imeanza mchakato wa ujenzi wa kituo jumuishi cha huduma za parachichi ambacho kitasaidia kuhifadhi na kuchakata  zao la Parachichi kitakachojengwa eneo la Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

Haya yamesemwa jana (Jumamosi Mei 11, 2024) na Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Enock Nyasebwa ambaye alikuwa akijibu swali la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kiwira, wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto ya kuharibika kwa parachichi za wakulima katika eneo hilo, Bw. Nyasebwa alisema kuwa wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kimkataba ili kumuwezesha mkandarasi kuanza ujenzi.

"Ujenzi wa kiwanda hiki utawezesha kuongeza thamani ya zao la parachichi kwani itawezesha wakulima kuhifadhi mazao yao katika chumba baridi pamoja na kuchakata mazao yatokanayo na matunda hayo ikiwemo mafuta".

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika kuhakikisha wanaongeza thamani ya zao hilo, wameanza mpango wa kuweka vigezo ili kuhakikisha miche inayopandwa inakidhi, lengo likiwa ni kupata zao lenye ubora ambalo litafanya vizuri kwenye soko la kimataifa na kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi huyo ahakikishe wanakamilisha taratibu zilizobaki ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu kilimo bora cha zao la parachichi ili kuongeza thamani na ubora.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Busokelo lililoko eneo la Lwangwa na kuweka jiwe la msingi kwenye jengo hilo.

Mapema, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Busokelo, Bi. Loema Peter alimweleza Waziri Mkuu kwamba ujenzi wake umefikia asilimia 94 na akaomba Serikali ikamilishe taratibu za upatikanaji wa sh. bilioni 2.3 ili waweze kukamilisha hatua iliyobakia.

Alisema hadi sasa wamekwishapokea shilingi bilioni 6.08 za ujenzi na shilingi milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa samani za ofisi hizo.

(mwisho)