Habari
Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini-Dkt. Mwigulu
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Januari 18, 2026 ameshiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu Anglikana la Roho Mtakatifu Dodoma na amesisitiza kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na viongozi wa dini kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu, upendo, haki na uwajibikaji.
“Sote tunatambua kwamba Taasisi za dini zina nafasi ya kipekee ya kuhubiri na kufundisha maadili ya upendo, uvumilivu na kuheshimiana, ambazo ni nguzo kuu za amani ya Taifa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassananatambua na kuthamini sana mchango mkubwa wa taasisi za dini ikiwemo Kanisa la Anglikana, katika kudumisha amani, maadili mema na mshikamano wa Kitaifa.
Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa ibada za Jumapili ni sehemu muhimu ya maisha ya Mkristo na ni muda wa kujitathmini, kuimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu, na kujifunza namna bora ya kuishi kwa mujibu wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika familia, jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema Watanzania wanakumbushwa kuishi kwa misingi ya upendo, unyenyekevu, haki na uwajibikaji kwani Biblia inasisitiza wazi kuwa “Umejulishwa, ee mwanadamu, yaliyo mema; na Bwana anataka nini kwako, ila kutenda haki, kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu mbele za Mungu wako” (Mika 6:8) na maadili hayo si ya kidini pekee, bali ni msingi muhimu wa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema Tanzania imeendelea kuwa kielelezo cha amani, umoja na mshikamano katika ukanda wetu na barani Afrika. “Amani hii si jambo la bahati, bali ni matokeo ya jitihada za pamoja za Serikali, taasisi za dini, familia na wananchi kwa ujumla.”
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa imani wanayojifunza na kuimarisha katika ibada inapaswa kutafsiriwa katika matendo ya uadilifu, uwajibikaji, bidii katika kazi, kuheshimu sheria na kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa lenye haki, amani na maendeleo endelevu. “Imani ya kweli inapaswa kuonekana kwa matendo.”
Kadhalika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waumini wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuwa mabalozi wa amani katika familia zao, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla kupinga vitendo vyovyote vya chuki, migawanyiko na vurugu.
Awali, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani ameipongeza Serikali kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kidini likiwemo Kanisa Anglikana na kwamba wapo pamoja na nayo katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani. “Tunataka nchi iwe na amani ili shughuli ziendelee na hatutachezea amani.”




