Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Sera za Kisekta Zatakiwa Kuendana na DIRA 2050


Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imewakumbusha wataalamu wa uchambuzi wa sera nchini kuimarisha jitihada za kuhakikisha sera zote zinaendana na Dira 2050 ili kuwezesha utekelezaji wenye tija na kuleta matokeo tarajiwa kwa wananchi.

Wito huo umetolewa leo Juni 8, 2026 Jijini Arusha na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Uratibu wa Shughuli za Serikali, Bw. Paul Sangawe, alipokuwa akifungua kikao kazi maalum cha kuwajengea uwezo wataalamu wa uchambuzi wa sera kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Bw. Sangawe amesema kuwa, sera zina mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa, hivyo ni muhimu kuendana na Dira 2050.

“Ni muhimu sera zetu ziendane na Dira 2050 ili kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa hai na matokeo yanayokusudiwa yanaonekana kwa wananchi na taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Sangawe.

Aidha, ameipongea Taasisi ya Uongozi kwa mchango wanaotoa katika kuratibu sera na kujenga uwezo wa wataalam wa uchambuzi wa sera. 

Katika kikao kazi hicho, mada mbalimbali zimewasilishwa ikiwemo Dira 2050, hatua iliyofikiwa katika mapitio ya sera, nafasi ya sheria katika utekelezaji wa sera na uzoefu kutoka nchi nyingine.

Washiriki wa kikao hicho kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali wameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuandaa mafunzo hayo na kueleza umuhimu wa mafunzo hayo kuwa endelevu. Aidha, akitoa ufafanuzi Mkurugenzi alieleza kuwa, mafunzo hayo yatakuwa endelevu. 

Vilevile, amewahakikishia wajumbe hao kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushirikiana na wadau wote ikiwemo Tume ya Mipango katika kuhakikisha uratibu wa sera unaimarishwa nchini.