Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Dkt. Mwigulu ahitimisha ziara ya kikazi Iringa


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Iringa kwa kuwataka viongozi na watumishi wa umma kuendelea kusimamia haki, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
 
Mheshimwa Dkt. Mwigulu pia amewataka viongozi nchini wawaelimishe wananchi umuhimu wa kuandikishana mikataba wanapopeana ardhi badala ya kuendelea kufanya hivyo kwa kuaminiana.

"Viongozi mliopo hapa waambieni wananchi hivi sasa masuala ya ardhi wasifanye kwa kuaminiana, wawe wanaandikishana kwa mikataba na tena katika ofisi za kijiji ili watambulike," amesema. 

Ametoa wito huo leo (Jumapili, Juni 7, 2026) wakati akizungumza na viongozi wa kada mbalimbali wa mkoa wa Iringa katika kikao cha majumuisho ya ziara zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, mjini Iringa. 

"Ninawasihi wananchi tusiogope kurasmisha mambo yetu kwa sababu uaminifu unaenda unapungua. Tunaporasmisha, tunaepusha migogoro siku za usoni," amesisitiza. 

Waziri Mkuu ametoa rai hiyo kutokana na wingi wa kero zinazojitokeza kwenye mikutano aliyoishaifanya na hasa kwenye sekta ya ardhi. 

Amewataka viongozi wanapotaka kufanya uendelezaji wowote nao pia wahakikishe wanawapa wananchi husika mikataba ili kulinda haki yao

Akizungumzia utendaji wa watumishi wa umma, Dkt. Mwigulu alisema ni muhimu kuwatambua na kuwathamini watumishi wanaofanya kazi kwa uadilifu na ufanisi huku hatua stahiki zikichukuliwa kwa wale wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao.
 
“Haki, uwajibikaji na huduma bora kwa wananchi lazima viwe msingi wa utendaji wetu. Wananchi wanatarajia kuona matokeo ya kazi zetu na ndiyo dhamira ya Serikali,” alisema.
 
Aidha, Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa mkoa huo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo ikiwemo migogoro ya ardhi, madai ya wananchi dhidi ya taasisi na kampuni mbalimbali, pamoja na masuala ya ustawi wa jamii yaliyowasilishwa katika mikutano ya hadhara.
 
Kwa upande wa miundombinu, Waziri Mkuu alielekeza kuharakishwa kwa utekelezaji wa miradi ya barabara iliyo katika hatua mbalimbali za maandalizi na utekelezaji huku akisisitiza ujenzi wa miundombinu yenye viwango vinavyoweza kuhimili changamoto za mazingira.
 
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James alisema ziara ya Waziri Mkuu imeimarisha ari ya uwajibikaji kwa viongozi na watumishi wa umma pamoja na kutoa mwelekeo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.