Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Rais Samia, Dkt. Biteko wamlilia Nyamo - Hanga


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa waombolezaji wote kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo - Hanga kilichotokea Aprili 13, 2025 Bunda mkoani Mara.

Pia ameahidi kuwa Serikali itahakikisha kazi nzuri alizokuwa anazifanya Mhandisi Nyamo- Hanga inaendelezwa ili kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 16, 2025 katika kijiji cha Migungani, Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara wakati akiongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Umeme Tanzania, Mhandisi Gissima Nyamo - Hanga

“ Mhe. Dkt. Samia  alimpenda sana kijana wake hata msiba ulipotokea alinipigia simu na ameniagiza nisimamie vizuri msiba huu kwa vile amesema angependa kuona Gissima anazikwa kwa heshima,” amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza “ Mhe Rais ameniqmbia Mhandisi ameondoka lakini kazi alizofanya zitaendelea na bila shaka atawaletea TANESCO mtu mzuri atakayeweza pia kuliongoza Shirika na Serikali itahakikisha mipango na  malengo yote yanaendelezwa,”

Dkt. Biteko ameendelea kwa kuwaasa viongozi kuishi kwa kuwa baraka kwa wengine na sio kuwasababishia maumivu huku akisema  wasiwe vitunguu kwa kuwatoa machozi wengine.

Amesema “ Kwa niaba ya Mhe. Rais Samia ndugu zangu waombolezaji na familia naomba mpokee salamu za pole na na sisi Wizara tutaenzi mchango wake kwa kuendeleza yale mazuri aliyoyafanya,”

Dkt. Biteko amemuelezea Mhandisi Nyamo - Hanga kama kiongozi mtulivu na muadilifu na aliyewaunganisha pamoja wafanyazi wa TANESCO “Gisimma  alikuwa mtu anayekuja mbele yako akiwa na majibu ya tatizo unalokusudia, hakuwa mtu wa kulalamika mara nyingine  hata walipokosea watendaji aliowaongoza alikuwa tayari kupokea changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi. Binafsi nilimpenda sana,”

Aidha, amesema baada ya kuwa na umeme wa kutosha nchini, Mhandisi huyo aliongoza majadiliano ya kuuziana umeme na nchi ya Zambia.

Vilevile, ameiomba familia ya Mhandisi Nyamo- Hanga kuishi kwa umoja na upendo miongoni mwao.

Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Mhe. Profesa Sospeter Mhongo akizungumza kwa niaba ya wabunge amesema kuwa Mhandisi Nyamo - Hanga  alishirikiana na wenzake kupendekeza kuweka umeme kwa gharama ya shilingi 127,000/= badala ya shilingi 300,000/=. 

Marehemu alikuwa na uwezo mkubwa na hivyo nchi imepoteza bingwa aliyeweza kusimamia usambazaji wa umeme kwa gharama nafuu.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi amesema kuwa wananchi wa Mkoa huo wamepata pigo kubwa. Aidha, ametoa pole kwa familia ya marehemu, TANESCO na Wizara ya Nishati.

“ Nawaomba niwakumbushe watumiaji wa barabara kutumia barabara vizuri ili kuepusha ajali, natoa agizo kwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Mara la kuendesha operesheni ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika vizuri,” amesema Kanali Mtambi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa msiba huo umeigusa Wizara yake na katika kuenzi mazuri aliyoyafanya atahakikisha Wizara  inaendelea kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana ili kusaidia Watanzania kutumia nishati hiyo kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania, Dkt. Rhimo Nyansaho  ametoa pole kwa familia kwa kuondokewa na mzazi na pia amesema wamepata faraja kuona Watanzania wengi wamejotokeza kuaga mwili wa marehemu.

“ Alijiongezea ujuzi wa kusoma kozi za sheria na biashara ili aweze kujiongezea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi wakati wa kutekeleza majukumu yake,” amesema Dkt. Nyansaho.

Akiendesha ibada ya mazishi  ya mazishi ya marehemu Nyamo- Hanga, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Mkoa wa Mara, John Mwita Maguge  amewataka wanafamilia kuwa na faraja na kujipa moyo kwa kuwa huo ni mpango wa Mungu.

“ Niwaombe kuwa Mungu atawafuta machozi ili muendelee kushikamana. Mungu wetu wa mbinguni awe pamoja  na famia hii, wakati huu ni wa kwaresma hivyo wote tutubu na tumwamini yesu,” amesema

Ameongeza “Niwakumbushe Watanzania kuwa mwaka huu ni wa kuchagua Rais, wabunge  na madiwani hivyo tuhakikishe tunatumia nafasi hii ya kuchagua viongozi waadilifu na waaminifu,”

MWISHO