Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Rais Samia Awahakikishia wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Tafara ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro kuwa shughuli zote za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,  unaotarajiwa kufanyika Novemba, 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 zitaendelea kama ilivyokuwa awali kwa kuzingatia taratibu na mipaka ya Vijiji na Vitongoji iliyokuwepo awali kwenye maeneo yao.

Maagizo hayo yametolewa  na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. William Lukuvi kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Oloirobi, ambapo amewataka wananchi hao kuondoa hofu na wasiwasi badala yake kuendelea kuishi kwenye maeneo yao kwa amani, kwa kuwa nchi yao ya Tanzania ni Nchi ya amani na utulivu, inayowajali wananchi wake, kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na usawa.

Akiwasilisha ujumbe huo, amesema kuwa, Mhe. Rais amepokea kero na malalamiko kutoka kwa Viongozi na Vyombo vya habari na kuwaagiza askari wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutowanyanyasa wananchi pamoja na kuheshimu Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizopo, kwani Mhe. Rais Samia bado anatambua uwepo wa Serikali za Vijiji na Vitongoji vya maeneo ya Tarafa ya Ngorongoro.

Kwa upande wake Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda licha  ya kuwashukuru wananchi kwa uvumilivu na imani yao kwa Serikali, amemuhakikishia Waziri Lukuvi kuwa atasimamia maelekezo yote yaliyotolewa kwake, akiahidi pia kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizokuwa zimesimama ama kusuasua hasa katika Sekta ya Afya na Elimu zinarejea katika ubora wake na kwa viwango vinavyohitajika.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lukuvi ameambatana na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula pamoja na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania CP Awadh Juma Haji pamoja na Viongozi wengine wa Serikali na wa Chama Cha Mapinduzi CCM.