Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Watanzania tuendelee kushikamana


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana katika kipindi hiki ambacho dunia ina mahangaiko makubwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi.

“Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyotusisistiza na tuendelee kuiamini Serikali na jitihada za viongozi wake.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo  leo (Jumatatu, Februari 22, 2021) wakati aliposhiriki mazishi ya mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Lindi na Mtwara Ally Nalaga yaliyofanyika Mnazimmoja Lindi.

Amesema magonjwa hayo yameleta tafsiri tofauti na wakati mwingine kutokuwa na utulivu kwani watu wanatishana sana, hali ambayo inawafanya wasiwe na amani na kuwajengea hofu.

Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa aina zote za magonjwa ambayo yanawakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatafutia tiba. Hata hivyo, amewasisitiza wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kila ugonjwa. “Ukisikia UKIMWI kuna tahadhari zake, ukisikia kipindupindi kina tahadhari zake.”

Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini zote nchini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake ili liendelee kuwa na amani na kimbilio kwa walipoteza amani.

Akimzungumzia marehemu Nalaga, Waziri Mkuu amesema alikuwa mcheshi na mwenye upendo kwa kila mtu na alijitoa sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii. “Tumepoteza mtu muhimu kwenye jamii yetu ya wana-Lindi na Mtwara. Bwana Nalaga ametuachia mambo mengi hivyo tumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.”

Waziri Mkuu amewaasa wananchi wayaenzi mambo yote mema aliyoyafanya enzi za uhai wake ikiwa ni pamoja na kujitoa katika shughuli za maendeleo ya jamii.