Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Uwekezaji nchini hautakwama


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili kuhakikisha uwekezaji wao haukwami bali unakua na kuleta tija.

Amesema hayo jana (Novemba 28, 2022) alipotembelea na kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha  kutengeneza mabati cha Lodhia kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani.

Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wawekezaji nchini wanapata faida “tunathamini uwekezaji huu, tunaheshimu uwekezaji huu na tutakuunga mkono kwenye uwekezaji”

Amesema kuwa Wawekezaji wamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, elimu, kilimo, mawasiliano na hata ajira “ Upanuzi wa kiwanda hiki ni kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada zake za kuendelea kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa watanzania”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa uwepo wa wawekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda wanaisaidia nchi kwa kiasi kikubwa  kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje pekee “Leo hii hatuna haja sana ya kuagiza nondo Ulaya au Asia, nyingi zinapatikana hapa nchini ikiwemo kwenye kiwanda hiki cha Lodhia”

Aidha Waziri Mkuu amewataka wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu ili kuhakikisha malengo ya muwekezaji yanatimia “Endeleni kufanya kazi vizuri kwenye kampuni hii, ninyi ni mabalozi wetu wazuri”