Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Tunataka kuona miradi itokanayo na makusanyo ya ndani


MAJALIWA: TUNATAKA KUONA MIRADI ITOKANAYO NA MAKUSANYO YA NDANI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam na ya wilaya ya Kinondoni ambapo pamoja na mambo mengine ameagiza makusanyo ya fedha za ndani yatumike katika ujenzi wa miradi ya maendeleo badala ya kutegemea fedha zinazotoka Serikali Kuu pekee.

“Mwaka 2020/2021 mlikusanya zaidi ya shilingi bilioni 40, pamoja na makusanyo hayo makubwa lakini hatuoni mradi mkubwa unaotekelezwa kupitia fedha hizo. Makusanyo ya mapato na matumizi yasimamiwe vizuri na fedha hizo zitumike katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.”

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumatatu, Julai 11, 2022) wakati akizungumza na  viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na wa wilaya ya Kinondoni katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Dar Es Salaam.

Katika ziara hiyo yenye lengo la kukutana na viongozi na watumishi wa umma mkoani Dar Es Salaam ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwahamasisha kufanya kazi wa bidii, Waziri Mkuu amewasisitiza wasimamie vizuri maeneo yao na wafanye kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Sinza/Ng’ombe na Mfereji wa Kiboko katika eneo la Mtogole ambapo amewataka wananchi wa maeneo hayo kutunza mazingira na wahakikishe hawamwagi taka ndani ya mfereji huo.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Kinondoni ufanye maboresho ya mradi huo kwa kujenga madaraja madogo madogo yatakayowezesha mtu kutoka upande mmoja wa mto kwenda mwingine, pamoja na kuweka taa katika barabara hiyo.

Baada ya kukagua mradi huo, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya miradi ya ujenzi wa soko la wamachinga katika eneo la Mwenge pamoja na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Manispaa ya Kinondoni.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa ambaye ameambatana na Waziri Mkuu katika ziara hiyo amemuhakikishia Waziri Mkuu kwamba TAMISEMI kwa kushirikiana na viongozi wa mkoa huo watahakikisha maelekezo aliyoyatoa wanayafanyia kazi.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Amos Makala alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii ikiwemo ya afya na elimu.

“Mkoa umepokea jumla ya shilingi bilioni 4.5 zinazotokana na tozo ya miamala ya simu kwa ajili ya kuendeleza miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya, fedha hizi zimegharamia ujenzi wa majengo mapya ya wagonjwa wa nje na zahanati, upanuzi wa miundmbinu ya zahanati na vituo vya afya”