Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Tumedhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa mradi wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana Ruangwa na kusema Serikali imeadhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike ili kumuwezesha atimize ndoto zake kielimu.

Baada ya kukagua mradi huo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na maendeleo yake na amewataka waliokabidhiwa jukumu la kusimamia ujenzi huo waendelee kuwa waaminifu na wahakikishe wanashirikiana vizuri na mjenzi ili akamilishe kwa wakati.

Waziri Mkuu amefanya ukaguzi huo leo (Ijumaa, Februari 26, 2021). Shule hiyo ya mchepuo wa sayansi inajengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa kupitia fedha za mpango wa lipa kwa matokeo (EP4R), ambapo awamu ya kwanza imegharimu sh. milioni 700.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kunatarajiwa kuinua kiwango cha ufaulu kwa mtoto wa kike ambaye ni mlengwa. ”Tumedhamiria kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa kike kwa kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia. Tunataka watoto wa kike wasome bila usumbufu.”

Waziri Mkuu amesema walianzisha ujenzi wa shule ya wasichana katika wilaya hiyo ili kutoa fursa kwa mtoto wa kike ya kusoma vizuri akiwa katika mazingira rafiki yatakayomuepusha na changamoto mbalimbali zinazowafanya washindwe kutimiza ndoto zao kielimu.

Kwa upande wake, fundi mkuu wa mradi huo, Michael Fabian amesema shule hiyo inajengwa kwa awamu mbili na ya kwanza inahusisha jengo la utawala, vyumba vinane vya madarasa, nyumba mbili za walimu, matundu 16 ya vyoo, jengo la maabara za fizikia, kemia, baiolojia na jengo la jiografia.

Shule hiyo inatarajiwa kufunguliwa mara baada ya kukamilika kwa majengo ya awamu ya pili. Awamu ya pili ya mradi huo unaojengwa kwa kupitia mfumo wa force account , inahusisha mabweni, bwalo la chakula na kichomea taka.

Baada ya kukagua mradi huo wa shule maalumu ya sekondari ya wasichana Ruangwa, Waziri Mkuu alitembelea shule ya sekondari ya wasichana ya Liuguru iliyopo kata ya Narung’ombe ambapo alizungumza na walimu na wazazi na kuwasisitiza wanafunzi wazingatie masomo.

Waziri Mkuu amesema suala la mtoto wa Kitanzania kwenda shule ni la lazima na si hiyari,  hivyo wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda shule na watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao shule watachukuliwa hatua za kisheria. Serikali imeondoa michango yote ya hovyo ili kutoa fursa ya watoto kusoma.”

Awali, Waziri Mkuu alitembelea shule ya msingi Chikoko iliyoko katika kata ya Makanjiro ambapo amewataka wananchi washikamane na wajitokeze kwa wingi katika utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa madarasa.

Naye, Diwani wa kata hiyo, Simon Machela alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba atashirikiana na uongozi wa wilaya pamoja na wananchi wa kata hiyo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

-Mwisho-