Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Serikali itajenga 'Cold Room' uwanja wa ndege Songwe


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inatarajia kujenga chumba maalumu cha kuhifadhi baridi (cold room) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kuhifadhia maparachichi pamoja na mazao mengine kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 12, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kutembelea shamba la mkulima wa parachichi  Bw.  Steven Mlimbira katika kijiji cha Maheve wilayani Njombe.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Njombe zinazolima zao la parachichi zianzishe vitalu vya kuotesha miche katika eneo la kuanzia ekari tatu na kuigawa bure kwa wakulima, lengo likiwa ni kuhamasisha wananchi wengi kulima zao hilo na kuongeza uzalishaji. 

Kufuatia umuhimu za zao hilo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Mwita Rubirya afuatilie maendeleo ya vikundi vya wakulima wa parachichi na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Waziri Mkuu amesema zao la parachichi ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa na linazalishwa  kwa  gharama nafuu, hivyo amewahimiza wananchi kulima zao hilo kwa ajili ya kujipatia fedha zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.

Amesema zao la parachichi limechangia katika kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu wengi wameweza kujiajiri na kuajiriwa, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata zao hilo kwa kuwa linafaida kubwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amempongeza Bw. Mlimbira kwa kuwa na shamba kubwa la parachichi ambalo limewezesha kutoa ajira kwa wananchi wengi pamoja na kuwahamasisha walime zao kwa kuwagawia miche kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake, Bw. Mlimbira amesema ekari moja hupandwa miti 64 ya parachichi kwa nafasi ya mita nane kwa mita nane na mche mmoja huuzwa kati ya shilingi 2,000 hadi 5,000 kwa kutegemea na ukubwa wa mche.

Amesema mti mmoja wa parachichi unatoa kiasi cha wastani wa kilo 150 hadi 500 ambapo inakadiriwa kuzalisha parachichi zenye thamani ya shilingi 200,000 hadi 750,000 kwa mti wenye umri wa miaka mitano hadi 10 na huanza kuzaa baada ya mwaka mmoja na nusu hadi miaka mitatu.