Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

OFISI YA WAZIRI MKUU

Habari

Majaliwa: Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ujasiriamali


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na mkakati wa kufungua milango ya ujasiriamali kwa kutekeleza sera na programu mbalimbali zitakazowasaidia wananchi kuendana na soko la ajira ili kujiongezea kipato.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi Machi 13, 2025) alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya Amali ya Makomelo iliyopo Nzega mkoani Tabora ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 1.6.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali iliamua kutenga kiasi cha shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya ujenzi shule za amali katika kila mkoa ili kuwawezesha Watanzania kupata elimu ya mafunzo maalum yatayowasaidia kujiajiri au kuajiri wengine na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

“Lengo letu ni kupanua na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia sambamba na kutoa elimu yenye ujuzi na vitendo vyenye kukidhi katika ulimwengu wa ajira.”

“Malengo ya Serikali ni kuwafikisha vijana kupata ujuzi ili ujuzi huo utumike katika kujipatia kipato na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, na bahati nzuri sera yetu ya elimu imesisitiza elimu ya ufundi mahiri na tunaita amali.”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iliendesha mafunzo ya ufundi mahiri kwa vijana wenye uhitaji kwenye fani mbalimbali kwa kuwapeleka kwenye vyuo vikiwemo vya sekta binafsi ili kuwafanya wawe mahiri kwenye maeneo wanayoona yanaweza kuwaongezea kipato.

“Kwenye elimu tumefanya maboresho ya sera na tumegundua kuwa vijana wengi nchini wamemaliza ngazi mbalimbali za elimu na Serikali tunawajibika kuwatafutia fursa za kujiendeleza ikiwemo na vipaji vyao tukaamua kufanya tafiti ili kufahamu nini tufanye kwa pamoja kukabiliana na tatizo la ajira”

“Baada ya kufanya tafiti  ya namna ya kuboresha eneo la ajira kwa vijana,ambapo vijana wenyewe walishirikishwa na  sehemu kubwa ya maoni yao walishauri kujikita kwenye ufundi mahiri kwa kuanzisha mafunzo maalum ya ufundi kwenye ngazi mbalimbali.”

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kufanya sensa ya wazee katika eneo hilo na kuhakikisha wanafungua dirisha maalum ya kuwahudumia

“Serikali imetoa maelekezo ya wazee kutambuliwa na kila halmashauri kwa kupewa vitambulisho ili waweze kupata huduma bure, wekeni dirisha maalum, fanyeni sensa ya wazee kwa vigezo vilivyopo ili wazee hawa muwayambue na wahudumiwe”

Naye Mbunge wa Jimbo la Bukene Selemani Zedi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo kwenye sekta za maji, elimu, afya na miundombinu.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alizindua kituo kipya cha Mabasi cha Nzega mjini mkoani Tabora ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 4.327.

Akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho ambacho utekelezaji wake umefikia asilimia 100, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza halmashauri hiyo kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo hicho kwani kitaibua fursa za biashara kwa wakazi wa eneo hilo. “Kituo hiki ni kizuri na kimejengwa kwa ubora, kituo hiki kinatakiwa kianze kutumika ili wananchi waanze kunufaika nacho. Watumishi wa halmashauri ongozeni Wana-Nzega kunufaika na fursa katika eneo lenu.”